NA MAULID YUSSUF WEMA 

TUME ya Vyuo vikuu vikuu Tanzania (TCU) imesema ipo haja kwa Wanafunzi wa kidato cha sita kupewa Elimu ya namna ya kujiunga na Vyuo vikuu mbali mbali vya ndani na nje ya nchi.   

Akizungumza katika hafla ya Wiki ya juma la Elimu ya Juu katika viwanja vya Mapinduzi Square Kisonge, Afisa Udahili kutoka TCU, Estomii Edward, amesema Wanafunzi wengi wamekuwa wakijiunga na Vyuo bila ya kujua Chuo hicho kimesajiliwa  kutoa fani wanayoitaka au hakijasajiliwa.

Amesema ni vizuri Wanafunzi kuangalia mitandao ya TCU ili wajue Vyuo vipi vimesajiliwa na vipi bado havijasajiliwa ili kuepuka usumbufu wa kutojulikana vyeti vyao mara bada ya kumaliza masomo yao.

Nae Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, Aidha Maoulid Juma, amesema lengo la kuandaa juma la wiki ya Elimu ya juu ni kuhakikisha kuwa Wanafunzi wanapata taaluma ya kujiunga na Vyuo vikuu.

Hata hivyo, Aidha amewashukuru Walimu wa Kidatu cha sita na Wanafunzi  mbali mbali kwa kujitokeza kwa wingi katika hafla hiyo hali ambayo imewapa moyo ya kufikia malengo ya Juma hilo la wiki ya Vyuo vikuu. 

Nao baadhi ya Wanafunzi na wahitimu wa kidatu cha sita kutoka Skuli mbali mbali, wameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kuandaa juma hilo la wiki ya Elimu ya juu, kwani imewasaidia sana  kujua namna ya kujiunga Vyuo vikuu pamoja na kuvitambua Vyuo ambavyo vimesajiliwa na Tume ya Vyuo vikuu Tanzania.