Alikuwa mtumiaji dawa za kulevya, jambazi maarufu
Maisha ya ujana yaliishia kubadilisha jela mbalimbali
Kwa sasa ana mamilioni ya mashabiki ulimwenguni
DANNY Trejo ni mmoja miongoni mwa wacheza filamu zenye kuvutia na amejikusanyia mamilioni ya mashabiki pande mbalimbali duniani kutokana na kucheza mamilia ya filamu.
Kabla ya kujipatia umashuhuri kwenye filamu, Trejo kwenye maisha yake alilazimika kupandisha na kushusha milima na mabonde na kama si ujasiri, hakika tusingekuwa tunayasimulia mafanikio ya maisha yake aliyokuwa nayo.
Alizaliwa Mei 16 mwaka 1944, katika mji wa Echo Park uliopo karibu na jiji la Los Angeles, huko California, ambapo baba yake Dan Trejo ni fundi ujenzi na mama yake Alice Rivera ana asili ya nchini Mexico.
Katika miaka ya utoto, Trejo alikuwa mmoja kati ya watoto watukutu sana mitaani, hali ambayo ilisababisha mara nyingi kujikuta akiwa mikononi mwa polisi akikabiliwa na mashitaka ya uhalifu.
Alipofikia umri wa miaka miaka 20, Trejo alikuta akiishi jela mara kwa mara kutokana na kujihusisha na uhalifu ikiwemo matumizi na biashara ya kulevya, ujambazi ambapo alikuta akibadilisha jela za Folsom na San Quentin.
Kwenye maisha yake ya jela, Trejo alijishughulisha sana na mchezo wa ndondi na alinyakua mataji kadhaa kutokana na kufanya vizuri katika mchezo huo ambapo alikuwa akipiga kwenye uzani wa ‘lightweight’ na ‘welterweight’.
Moja ya lililomkuta kwenye enzi zake za maisha ya utukutu ni kupigwa risasi, lakini pia aliwahi kudungwa kisu, kukanyangwa kanyagwa na kukabiliwa na mateso.
Baada ya kujikuta akiwa mikononi mara kwa mara kwenye mikono ya polisi, Trejo alifikiria kuachana na shughuli za kihalifu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya ambapo alipata msaada wa kuachana na uraibu huo.
Wakati akifikiria kuachana na masuala ya uhalifu na kuwa mtu mwema katika jamii alianza kujishughulisha na kazi za kibarua kwenye kampuni za ujenzi na baada ya kuona hakuna maslahi ya kutosha akajitosa rasmi kwenye uigzaji filamu.
Katika filamu nyingi anazoshiriki, nywele zake ni ndefu na mara nyingi huwa zinasokotwa, mara nyingi huachilia kifua chake wazi kilichochorwa tattoo akionesha ubabe huku mikononi akiwa amechukua silaha.
“Nilipoanza kuwa maarufu, kuna rafiki yangu mmoja aliniambia, dunia nzima inaweza kufikiria wewe ni nyota wa filamu, lakini huwezi. Sitaki kuwa nyota wa filamu. Nataka kuwa mwigizaji mzuri tu”, alisema.
Alisema kwamba alipoanza kuigiza filamu, kila wakati alikuwa mhusika anayeishia gerezani na mfungwa namba moja kwa sababu ya muonekano wake na tabia zake zilivyokuwa.
Alikiri kwamba kabla ya kuingia kwenye uigizaji wa filamu, ukweli ni kwamba alijikuta akiwa mfungwa mara kwa mara kutokana na kujihusisha na vitendo vya kihalifu.
Hivi karibu Trejo alichapisha makala inayoitwa ‘The Rise of Danny Trejo’, ambayo inaelezea wasifu wa maisha yake hali ambayo inatoa nafasi watu wengi zaidi duniani kumfahamu.
“Ni miujiza kuzungumzia maisha yangu niliyonayo hivi sasa kwa sababu hata sikutakiwa kuachiliwa huru kwneye miaka ya 1960 kutokana na vitendo vya uhalifu nilivyovitekeleza”, alisema wakati alipokuwa akizungumza na radio 1 Newsbeat.
Akikumbukia ujana wake, Trejo alisema alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya katika miaka ya 1960 na ndani ya ndani ya gereza alikuwa anafahamika vyema, na akawa bingwa wa ndodi katika gereza kuu la San Quentin, gereza la zamani zaidi California.
Miongoni mwa mambo anayoyakumbuka kwenye maisha yake ya jela ni mmoja kati ya wafungwa wenziwe akidungwa kisu mgongoni.” Alikuwa anatembea upande wa juu wa bustani, akijaribu kufikia kisu huku akiwa anakohoa damu”.
Trejo pia aliwahi kufungwa katika magereza mengine mawili ya Soledad na Folsom na anakubali kwamba kushiriki katika kuanda makala ya maisha ya ujana wake inamuuma sana.
“Nakumbuka nikiwa mahabusu ya watoto Marekani na wakati huo nilifikiria kwamba sasa maisha yangu yameisha. Kwasababu hapo hapo ndani ya gereza utapata masomo pia. “Nikajaribu kusema hapana, subiri kidogo. Mambo bado. Hapa ndio mwanzo unaanza.”
Aliamua kubadili maisha yake kwa kuachana na dawa za kulevya, ambapo baada ya hapo akawa mshauri wa masuala ya dawa za kulevya na kuamua kutumia tajriba yake kusaidia wengine kabla ya kujiunga na tasnia ya filamu.
Na pia tangu alipoingia kwenye filamu amekuwa akijitahidi kuwa mwema kwasababu anafahamika fika kwamba umaarufu wake unaushawishi mkubwa na ana imani kwamba atahamasisha vijana wengine wengi mashabiki wake.
“Haijalishi unaanzia wapi, cha muhimu ni vipi mwisho wako utakavyokuwa.”
Katika makala, utamuona Trejo akiingia gerezani na kushirikisha wafungwa tajriba yake mwenyewe. Anasema kila wakati anapokuwa huko, anavuta harufu ya ‘uoga na wasiwasi’.
“Nilitoka gerezani na ninaota kwamba bado niko gerezani. Hilo linanifanya ghafla nina amka na linanikumbusha kwamba sistahili kwenda kinyume na sheria.”
Kadiri muda unayokwenda amekuwa na ratiba yenye sughuli nyingi za kikazi na kuna baadhi ya mashabiki wake wanauliza atastaafu lini kucheza filamu?
Lakini jibu lake lilikuwa fupi kwa mashabiki wake wenye masuali ya namna hiyo ambapo alisema, “sifikirii kama nitastaafu hivi karibuni, ninawakati mzuri sana”, alisema.
Kwa mujibu wa ripoti mcheza filamu huyo ana utajiri wa dola milioni 16, ambapo nyingi ya fedha hizo alizozikusanya zimetokana na kucheza filamu ambapo huigiza kama mpizani mkubwa wa steringi.
Katika maisha ya kisasa watu wengi hujikuta wakichora tattoo, ambapo kila mmoja hujichora kwa sababu mbalimbali, lakini kwa upande wa Trejo, tattoo kubwa aliyochora kifuani ni picha ya aliyekuwa mkewe anaitwae Debbie na mwanawe Danielle.
Tattoo hizo alizozichora kifuani zinathibitisha kuwa nguli huyo wa filamu nchini Marekani ni mtu anaijali na kuipa umuhimu mkubwa sana familia yake na kweli alipendana kiukweli na Debbie ingawaje kwa sasa hawapo pamoja.
Katika filamu nyingi hasa zile za kibabe na undava zinazochezwa na Trejo suala la kuigiza kuua na kufa ni jambo, hata hivyo kwa upande wake takwimu zinaonesha kuwa amekwisha igiza kufa kwenye filamu zipatazo 65.
Filamu yake ya kwanza kuigiza kufariki ilikuwa mwaka 1987 ambapo kwenye filamu hiyo alifariki wakati akijaribu kukimbia kwenye tukio la mripuko uliotokana na chupa za pombe.
Trejo anamiliki nyumba ya kifahari katika eneo la bonde la San Fernando, ambapo katika maisha ya ndoa aliyoifunga Disemba 12, 1997 na Debbie Shreve walijaaliwa kupata watoto wawili Gilbert na Dannielle.
Trejo na Debbie Shreve walifikia hatua ya kuvunja ndoa mnamo mwaka 2009, baada ya kushindwa kufikia suhulu kwenye matatizo yao yaliyokuwa yakiwakabili kama mke na mume.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Trejo ni baba wa watoto wawili wa kiume Danny Boy na Jose na mtoto mmoja wa kike aitwae Esmeralda ambapo watoto hawa alizaa kwenye mahusiano mengine nje ya ndoa yake.
Mbali ya Trejo kujulikana sana kwenye filamu, pia amekuwa akijishuhgulisha na kazi mbalimbali za ujasirimali ikiwemo kumiliki mikahawa yenye kutoa huduma za vyakula na vinywaji.
Katika jiji la Los Angeles, Trejo anamiliki mikahawa maarufu ukiwemo wa taco uliopo eneo la La Brea Avenue, pia anamiliki mikahawa katika mji ya Las Vegas na anamiliki shea kwenye kampuni mbalimbali.
Miongoni mwa filamu mashuhuri zinazopendwa alizocheza Danny Trejo ni pamoja na ‘Con Air’, ‘Zombie Hunter’, ‘3-Headed Shark Attack’, hata hivyo filamu zote hizo tatu Trejo anaishia kufariki.