WASHINGTON, MAREKANI

RAIS  Donald Trump wa Marekani amevaa barakoa hadharani kwa mara ya kwanza ikiwa ni ishara ya kusalimu amri kwa shinikizo la kumtaka kuwa mfano kwa umma wakati janga la virusi vya corona linaendelea kuitikisa Marekani.

Trump alionekana akiwa amefunika pua na mdomo kwa kutumia barakoa yenye nembo ya rais alipotembelea hospitali moja ya kijeshi nje kidogo ya mji mkuu Washington alipokwenda kukutana na maveterani waliojeruhiwa.

Ilielezwa kuwa wasaidizi wake walimuomba kiongozi huyo kuvaa barakoa hadharani katika kipindi ambacho visa vya virusi vya corona vinaongezeka katika baadhi ya majimbo nchini Marekani.

Trump ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa sharti la kuvaa barakoa, mara kadhaa alitetea jinsi utawala wake unavyolishughulikia suala la corona licha ya kwamba Marekani ndiyo taifa linaloongoza duniani kwa maambukizi pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19.