NA HAJI NASSOR

JUMUIYA ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE)imesema rushwa muhali na mashahidi kutokwenda mahakamani kutoa ushahidi, ndio tatizo linalosababisha kesi za udhalilishaji zichelewe kupatiwa hukumu.

Mratibu wa jumuiya hiyo, Tatu Abdalla Mselem, alisema serikali kwa nia nzuri ilizifanyia marekebisho sheria za ushahidi, sheria ya adhabu na ile ya mwenendo wa makosa ya jinai na kuweka adhabu kali wakosaji, lakini hayo yote yanategemea jamii kutoa ushidi.

Akizungumza kwenye mkutano wa masheha, waratibu wa wanawake na watoto wa shehia za Matale, Pujini, Uwandani, Mchangamrima na Wara wilaya ya Chake Chake, wanasheria, watendaji wa kituo cha mkono kwa mkono na madawati, alisema, uwepo wa sheria kali ni jambo moja na utekelezaji ni jambo jengine.

Alisema, majaji, mahakimu, waenedesha mashtaka, polisi na mawakili hawezi kufanya jambo lolote pindi ikiwa rushwa muhali itatawala katika jamii.

Alieleza kuwa, ni aibu baada ya serikali kwa kushirikiana na wadau kama asasi za kiraia hadi kufikia kuwa na sheria nzuri kwa wadhalilishaji, kisha waathirika wa matukio hayo wakashindwa kupata haki yao.

Aliwasisitiza masheha na waratibu wa shehia hizo, kuendelea kuwaelimisha wananchi kufika mahakamni kutao ushahidi na kukataa suluhu.

Alisema jumuiya yao inatafuata ufadhili kila kona ili kuhakikisha wanaisaidia jamii ya Pemba katika kutokomeza udhalilishaji.

Hata hivyo, aliwasisitiza wanasheria wanaoendesha kesi za udhalilishaji, kuhakikisha wanazitumia sheria kama zilivyo ikiwemo kutoa adhabu kali kwa wakosaji.

Katibu wa jumuiya hiyo, Ibrahim Omar Mohamed,alisema  makosa ya udhalilishaji ni rahisi kuondoka Zanzibar ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake.

Alieleza kuwa iwapo jamii itaachana na rushwa muhali na kufika mahakamani kutoa ushahidi na mahakimu na waendesha mashtaka kutimiza wajibu wao, udhalilishaji utakuwa historia.

Mapema wakili wa serikali  kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Juma Ali Juma, akiwasilisha mada ya ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto, alisema dawa ya kuondoa vitendo hivyo ni jamii kutoa ushahidi mahakamani.