NA TATU MAKAME

ZANZIBAR ni miongoni mwa nchi za Visiwa ambapo pamoja na mambo mengine inategemea shughuli za utalii kwa ajili kujipatia fedha za kigeni.

Utalii wa Zanzibar umeanza mnamo miaka ya 1990 mara baada ya kuanguka kwa soko la zao la karafuu duniani ambapo hapo kabla lilikuwa ni zao kuu la bishara linaloiingizia nchi fedha za kigeni.

Madhari ya Visiwa hivi yamekuwa na muonekano wa kipekee ukilinganisha na nchi nyingi duniani zikiwemo zile za bara la Ulaya na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Visiwa hivi vinatembelewa na watalii kutoka nchi mbalimbali duniani wanaofika kujionea vivutio vilivyopo ambapo wakifika Zanzibar hutembezwa na kundi la vijana wanaoitwa ‘mapapasi’ ambao hufanya kazi ya kutembeza wageni hao.

Awali kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na kundi la vijana wanaume pekee lakini kwa kutokana na mambo kubadilika kila chuo hivi sasa shughuli hiyo inafanywa na vijana wa kike.

Kama inavyojulikana kuwa wanawake wanaweza bila ya kuwezeshwa ndivyo ilivyo kwa watembeza watalii hao wa kike ambao wanaimudu vyema kazi yao hiyo.

Kundi hilo linajuilikana kwa jina la ‘Zanzibar mamas’ chini ya Katibu Mkuu wake Sharon Robert Mhina kwa sasa wameshika hatuma ya kazi ya kutembeza watalii.

Lengo la kundi hilo kuanzisha ni kuisaidia serikali kutangaza utalii wa ndani kwa kuwa huwaelimisha wageni hao vivutio vilivyomo Zanzibar.

Ikumbukwe kuwa wageni wengi wanaokuja wamekuwa na mwamko mzuri wa kutembelea maeneo ya vivutio ingawaje wananchi wengi wa Zanzibar hawana mwamko wa kutembelea vivutio hivyo licha ya kuwa karibu navyo.

Washwahili wanasema “mgeni njoo mwenyeji apone” kuwepo kundi hili wanawake wengi watapata fursa ya kutembelea maeneo hayo hasa utalii wa ndani.

Aidha watalii wanawake na wao watapata muongozo wa kutembelea vivutio bila kutegemea kutembezwa na wanaume pekee ambao walikuwa wakiwatembeza wageni katika Mjimkongwe.