TUNIS,TUNISIA
WIZARA ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tunisia imetangaza kuwa, nchi hiyo itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tunisia ilisema kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Salma Neifer alifanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya akisisitiza udharura wa kuendelea kuungwa mkono Serikali ya Tripoli inayoongozwa na Fayes al Sarraj.
Salma Neifer alisema Tunisia inafanya jitihada za kupatikana utatuzi wa kisiasa nchini Libya na kuwepo uthabiti wa kiuchumi na kijamii nchini humo.
Pande hizo mbili zilitilia mkazo suala la kudumishwa mawasiliano na ushirikiano kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro wa Libya.
Libya ilitumbukia katika mapigano na mgogoro wa kisiasa mwaka 2011 baada ya Marekani na nchi wanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO),kufuata malalamiko ya wananchi na kumuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.
Kwa sasa nchi hiyo ina serikali mbili,moja ikiwa ile inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa yenye makao makuu huko Tripoli, mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj, na serikali yenye makao makuu katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi inayosaidiwa na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya.