NA HUSNA MOHAMMED

LEO ni sikukuu ya Eid el Hajj (Eid – el adh-ha) ambapo waislamu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanaungana na waislamu wenzao duniani kusherehekea sikukuu hii.

Sikukuu hii ni ya kuchinja ambayo huadhimishwa baada ya Waislamu kukamilisha ibada ya Hijja ambayo ni nguzo ya tano katika nguzo za Uislamu.

Sikukuu ya kuchinja (Eid el Adh-ha), au wengine huiita Idd kubwa, ni mojawapo kati ya sikukuu mbili kubwa kwa Waislamu. Moja ikiwa ni sikukuu ya kutoa Zakka – Eid el Fitr baada ya kumaliza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na ya pili ni hii ya kutoa kafara ya mnyama (kuchinja) baada ya kukamilisha ibada ya Hijja.

Sababu kubwa ya kuchinja ni kukumbuka majaribio aliyopewa Nabii Ibrahimu (AS) na Mola wake. Ibrahim alioteshwa amchinje mwanawe Ismail ambaye alimpata baada ya miaka mingi akiwa ameshakuwa mzee na baada ya kukata tamaa kabisa.

Wakati tayari ameshamwekea kisu shingoni Ismail, akabadilishiwa na kuwekewa mnyama aliyetoka mbinguni, hivyo badala ya kumchinja mwanawe, nabii Ibrahim akamchinja mnyama.

Katika sikukuu hii, Waislamu huadhimisha kwa kuchinja wanyama kama vile ngamia kondoo au mbuzi. Nyama inayochinjwa kama sadaka ya siku ya Eid el-Adh-ha zaidi hutolewa kwa watu wengine. Moja ya tatu huliwa na familia na jamaa wa karibu, moja ya tatu hutolewa kwa marafiki na moja ya tatu hutolewa msaada kwa maskini.

Ni muhimu kuelewa kwamba sadaka yenyewe, kama inavyofanywa na Waislamu, haihusiani kwa lolote na dhana ya kuondolewa dhambi wala kwamba kuzisafisha nafsi zao kutokana na dhambi: ﴾“… Si nyama zao au damu zao zimfikiazo Mwenyezi Mungu, bali ni uchamungu wao ufikao kwake﴿ (Quran 22:37).

Uislam unahimiza kuamrishana mema na kukatazana maovu, katika Uislamu siku ya sikukuu ni siku ya kumshukuru Mungu Muumba kwa neema alizowapa waja wake.

Anayediriki kuipata sikukuu anapaswa ashukuru kwa kufanya ibada kama vile kuswali, kutembelea wagonjwa, kutembelea wazee (ndugu, jamaa na marafiki), kuvaa nguo nzuri, kula chakula kizuri na kutoa sadaka na zakka.

Sikukuu zote mbili kuu katika Uislam (Eid es Fitr – sikukuu ya kumaliza mfungo na Eid el Adh-ha – sikukuu ya kumaliza ibada ya hijja) zimeambatana na kutoa zakka.

Eid el Fitr Waislam wanapaswa watoe zakka ya chakula (Zakatul Fitr) na kwamba bila ya kutoa zakka hiyo funga zao huwa zimening’inizwa (hazipokelewi).

Wakati wa Eid el Adh-ha wanapaswa watoe zakka ya nyama (kwa kuchinja mnyama kama vile ng’ombe, ngamia, mbuzi au kondoo) na kugawa nyama katika mafungu; kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kuwapa masikini na kuwapa majirani.

Hivyo sikukuu katika Uislam ni ibada, si siku ya kufanya uzinifu, kunywa pombe na kufanya kufuru. Ni siku ya kumtakasa Mwenyezi Mungu kwa sana na kuhudhuria katika vikao vya heri.

Ni siku tukufu ya kuombeana kheri, kusameheana na kujumuika pamoja kwa ndugu, jamaa na marafiki, kwenda katika kumbi za mambo ya kheri kwa kushirikiana kwa hali na mali.

Huku serikali katika sikukuu hii ya Eid El Adh-ha ikiwa imeruhusu watu kwenda viwanjani kusherehekea sikukuu hiyo baada ya kupungua kwa janga la corona hapaZanzibar ni vyema jamii ikachukua tahadhari ya hali ya juu ili kuepuka maambukizi mapya.

Aidha tunawashauri wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao katika viwanja vya sikukuu kwa lengo la kuwalinda na watu waovu kama wabakaji nakadhalika.

Aidha ni vyema kwa wazee na walezi kuepuka kuwavisha vitu vya thamani, jambo ambalo linaweza kupelekea kuporwa n ahata kuumizwa.

Pia ipo haja ya kuchukua tahadhari ya vyakula vya vimiminika kama vile maziwa, urojo, juisi nakadhalika kwa lengo la kujikinga na magonjwa ya mripuko kama kipindupindu na matumbo ya kuharisha.