WAISLAMU wa Zanzibar, leo wanaungana na waislamu wenzao duniani kote kusherekea sikukuu ya Eid al – Adha au kama inavyotambulikana kuwa ni Eid ya kuchinja.

Eid al – Adha inatukumbusha tukio la kiimani pale Mwenyezi Mungu alipoipima imani ya nabii Ibrahim (A.S) kwa kumuamrisha amchinje mtoto wake nabii Ismael.

Nabii Ibrahim akiwa anajiandaa kutekeleza amri ya Mwenyezi na kuonesha imani yake ni kubwa kwa Mwenyezi Mungu zaidi kuliko mwanawe, Mwenyezi Mungu alimletea mnyama kwa ajili ya kumchinja.

Kwa kawaida waislamu husherekea Eid al – Adha, kufuatia waumini wa dini hiyo kuwa kwenye hatua za mwisho za kuitekeleza ibada ya hijja huko katika mji mitakatafu ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia kuikamilisha.

Kwanza kabisa tunapaswa kuwaombea kila la kheri waislamu wenzetu waliojaaliwa kwenda kutekeleza ibada ya hijja na kuimaliza salama wakiwa wazima wa afya.

Ingawaje kwa mwaka huu ibada ya hijja imekubwa na mtihani wa kuwepo maradhi ya corona, kiasi kwamba mamlaka nchini Saudi Arabia zimelazimika kusitisha uingiaji wa mahujaji kutoka sehemu nyengine duniani.

Kwa mujibu wa taarifa Saudi Arabia nchi ambayo ina miji mitukufu kwa ajili ya ibada ya hijja, ni miongoni mwa nchi zilizoathirika na ugonjwa wa corona zaidi katika ukanda wa nchi za mashariki ya kati.

Taarifa rasmi kutoka katika nchi hiyo hadi Julai 29 ambayo ni siku ya kwanza ya ibada ya hijja mwaka huu, wananchi wapatao 270,831 wa Saudi Arabia wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa corona.

Aidha taarifa zaidi zinaeleza kuwa nchi hiyo imeshapoteza watu 2,789 kutokana na ugonjwa huo, huku wagonjwa 225,624 wakiripotiwa kupona baada ya kupata maambukizi ya corona.

Kwa mwaka huu kutokana na janga la virusi vua corona, imesababisha waislam wasiopindukia 10,000 pekee kuwa ndiyo waliohudhuria kushiriki tukio hilo kubwa la mkusanyiko wa kidini.

Kwa mwaka huu, Saudi Arabia imechukua theluthi mbili ya mahujaji waliochaguliwa mwaka huu ni wageni wanaoishi nchini Saudi Arabia na serikali imesema kuna uwakilishi wa mataifa 160 ambayo kwa kawaida waumini wake wa kiislamu kila mwaka hushiriki ibada hiyo.