LICHA ya kuwa Zanzibar imefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa miongo kadhaa lakini katika siku za hivi karibuni ugonjwa huo umeibuka tena hapa Zanzibar.
Kuweko kwa wagonjwa hao kunaturejesha kumbukumbu ya miaka ya nyuma ambapo watu wengi walikuwa wakiuugua ugonjwa huo na wengine wakipoteza maisha jambo ambalo serikali ililazimika kukaa chini ili kupambana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na wizara ya afya Zanzibar imesema kuwa imebaini kuwepo kwa wagonjwa wa malaria walioripotiwa katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja na vituo tofauti vya afya Unguja na Pemba.
Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu tumeambiwa kuwa watu wapatao 8,869 wameugua ugonjwa wa malaria visiwani Zanzibar.
Ofisi ya Tathmini wa Ufuatiliaji Kitengo cha kumaliza malaria Zanzibar, imetueleza kuwa wagonjwa 5,500 waliripotiwa kuanzia Januari hadi Machi na wengine 3369 waliripotiwa kuanzia Aprili hadi Juni.
Pia tathmini hiyo imetubainishia kuwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2019 Zanzibar iliripoti wagonjwa wa malaria 3,635.
Tumeelezwa kuwa utafiti uliofanywa mwaka 2017 ulionyesha kwamba utumiaji wa vyandarua upo chini kwa asilimia 59, hali ambayo inafanya kuongezeka kwa maradhi hayo, kutokana na hali hiyo inaonesha kuwa jamii zimeona kuwa ugonjwa huo haupo tena na hivyo kuregeza masharti ya kujikinga na ugonjwa huu.
Kwa kweli takwimu hizi zinaonesha Dhahiri ugonjwa huu upo katika jamii zetu na kwamba jitihada za makusudi zinahitajika kuutokomeza tena.
Kama tunavyofahamu kuwa ongezeko la wagonjwa hawa limesababishwa na kuwepo mazalia mengi ya mbu yaliyochangiwa na mvua za masika zilizomaliza hivi karibuni, hivyo tunakiomba kitengo cha kupambana na malaria kupiga dawa hasa maeneo yaliyoripotiwa wagonjwa wengi.
Sambamba na hilo lakini pia tunakiomba kitengo hicho kuendelea na utaratibu wake wa ugawaji wa vyandarua kwa lengo la kudhibiti tena malaria yasiweze kuleta athari katika jamii zetu.
Baadhi ya maeneo ambayo yamebainika kuwa na mbu wanaosababisha vimelea vya malaria kuwa ni pamoja na Chukwani, Shakani, Cheju na Kikwajuni mjini Unguja ambapo kwa kisiwani Pemba ni maeneo ya kaskazini Pemba ikiwemo eneo la Tumbe na maeno mengine ya visiwa hivi.
Aidha tunakishauri kitengo husika kuweka mikakati ya pamoja na kuelimisha tena jamii kujilinda na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kuwapima wananchi ambao katika maeneo yao kuna maambukizi mengi.
Mikakati mingine tunayoiomba kutekelezwa ni kugawa vyandarua kwa wananchi wote katika shehia na kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya kinga ya malaria.
Pia kuweko ufuatiliaji wa wagonjwa wa malaria majumbani baada ya kupata ripoti kutoka hospitali na vituo vya afya jambo ambalo litasaidia sana katika kupambana na ugonjwa huo.
Alitoa wito kwa wananchi kubadilika na kukubali kutumia vyandarua ili kujikinga na malaria kwa sababu ugonjwa huo bado upo.
Pamoja na mikakati hiyo tunaiomba jamii kuwa tayari kupokea maelekezo yote yatakayotolewa na kitengo husika cha malaria ikiwa ni pamoja na kukubali kupigiwa dawa, kuvitumia vyandarua watakavyopewa pamoja na kuweka mazingira yao katika hali ya usafi.