PARIS, Ufaransa

TUZO ya Ballon d’Or inayohusu wanasoka bora wa mwaka haitatolewa mwaka huu wa 2020 kutokana na janga la corona.

Waandaaji wa tuzo hiyo, France Football wametangaza uamuzi huo wakidai kwamba, hakutakuwa na usawa kutokana na ukweli kwamba janga la corona limesababisha ligi mbalimbali za soka kufutwa ndani ya msimu.

Tuzo hiyo imekuwa ikitoka kila mwaka tangu 1956, hivyo hii itakuwa mara ya kwanza kutofanyika.

Nyota wa Barcelona, Lionel Messi ndiye aliyeshinda tuzo hiyo mwaka jana kwa upande wa wanasoka wa kiume, wakati mshambuliaji  wa Marekani, Megan Rapinoe, alinyakua tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.

Kwa maana hiyo, Messi – ambaye amebeba tuzo hiyo mara sita ataendelea kutamba hadi mwakani.

Kwa mwaka huu, nyota  wa soka waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kunyakua tuzo hiyo ni mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski, kiungo mshambuliaji wa Manchester City, Kevin De Bruyne na  Sadio Mane, Virgil van Dijk na Mohamed Sala wa Liverpool.