BEIJING,CHINA

MSEMAJI wa Idara ya Takwimu ya Taifa ya China Liu Aihua amekutana na wanahabari na kusema, kutokana na mwelekeo mzuri wa hali ya kinga na udhibiti wa maambukizi ya virusi vya Corona, China imeharakisha hatua za kurejesha shughuli za kibiashara na uzalishaji mali.

Takwimu zilizotolewa na Idara ya Takwimu ya Taifa ya China zinaonesha kuwa, Pato la ndani la Taifa (GDP) katika nusu ya kwanza ya mwaka huu lilifikia yuan trilioni 45.66, ikiwa ni sawa na dola za kimarekani trilioni 6.52, ambayo imeshuka kwa asilimia 1.6 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Msemaji wa Idara ya Takwimu ya China  Liu Aihua alisema, uchumi wa China ulianza kukua kuanzia robo ya pili ya mwaka huu.

“Katika robo ya pili ya mwaka huu, pato la ndani la taifa liliongezeka kwa asilimia 3.2 kuliko mwaka jana kipindi kama hicho, na kuanza kukua baada ya kushuka kwa asilimia 6.8 katika robo ya kwanza ya mwaka, na vigezo vikuu vinaonesha kuwa uchumi umeboreka kuanzia robo ya pili ya mwaka.”alisema.

Msemaji huyo alisema, ukuaji huo haukupatikana kwa urahisi wakati China ilipokuwa inakabiliwa na changamoto kubwa ya janga la COVID-19 na mazingira ya kutatanisha ya ndani na nje ya nchi.

Takwimu zinaonesha kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, watu milioni 5.64 mijini walipata ajira, idadi ambayo ilifikia asilimia 62.7 ya lengo la mwaka mzima.

Liu Aihua alisema, serikali iliweka sera madhubuti za kuhimiza ajira na kuhakikisha maisha ya wananchi, ambazo zilionesha ufanisi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

“Katika miezi ya karibuni kiwango cha ukosefu wa ajira mijini kimeendelea kupungua, na kufikia asilimia 5.7 mwezi Juni.

Idadi ya watu wenye ajira ambao hawakuenda kazini katika kipindi cha COVID-19 pia iliendelea kushuka na kufikia asilimia 0.8 hadi kufikia mwezi Juni, ikiwa ni sawa na mwaka jana.

Hata hivyo, kutokana na sera za kuhimiza ajira, mabadiliko chanya kwa hali ya ajira yalionekana tangu nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Aidha, takwimu pia zinaonesha kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, sekta ya viwanda ya China ilirejesha uzalishaji hatua kwa hatua, mauzo ya mtandaoni yaliongezeka kwa kasi, na muundo wa biashara ya nje uliendelea kuboreka.

Mtafiti wa Ofisi ya Makonsela ya Baraza la Serikali la China Yao Jingyuan anaona kuwa, uchumi wa China utadumisha mwelekeo wa kufufuka katika nusu ya pili ya mwaka huu.