PARIS,UFARANSA

VIONGOZI wa Ufaransa, Ujerumani na Italia wametishia kutumia vikwazo dhidi ya mataifa yanayoendelea kukiuka marufuku ya Umoja wa Mataifa ya kuingiza silaha nchini Libya.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi wakuu wa mataifa hayo baada ya mkutano uliofanyika mjini Brussels, ilitoa wito kwa washirika wote wa kigeni kukomesha kuingilia vita inayoendelea na kuheshimu marufuku ya kuingiza silaha nchini Libya.

Rais Emannuel Macron wa Ufaransa,Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte walisema wako tayari kutafakari hatua za vikwazo iwapo uingizaji silaha kupitia majini, ardhini na angani utaendelea.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa mataifa hayo matatu kutishia kutumia vikwazo katika wakati ambapo wasiwasi unaongezeka kuwa machafuko zaidi yanaweza kutokea kwenye mzozo unaoendelea nchini Libya.