NA LAYLAT KHALFAN

HIVI karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir, alivunja mabaraza ya madiwani ya Manispaa na Halmashauri za wilaya zilizopo Unguja na Pemba.

Serikali inajivunia ushirikiano wa mabaraza hayo hasa pale serikali kuu ilipotoa maelekezo ambayo yalifuatwa na kuyafanyia kazi kwa kuzingatia sheria, sera na kanuni zinazosimamia uendeshwaji wa serikali za mitaa.

Nijambo la kufurahia kwa baadhi ya halmashauri kwa juhudi na kazi nzuri walizozifanya mpaka kupelekea kuomba kupandishwa hadhi kutoka halmashauri na kuwa mabaraza ya miji, serikali ilizingatia vigezo katika kupandisha hadhi halmashauri hizo.

Kama ilivyoelezwa katika sheria chini ya kifungu cha 14 (1) sheria ya Mamlaka za serikali za mitaa namba 7 ya mwaka 2014, vigezo hivyo vikiwa ni pamoja na kukua na kuimarika kwa huduma za kijamii, miundombinu ya mji, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu.

Kwa mnasaba huo hatuna budi kumpongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa uamuzi wake mzuri wa kuitangaza Zanzibar kuwa jiji na kupelekea Zanzibar kuwa miongoni mwa majiji yanayotambulika ulimwenguni.

Lengo la serikali kugatua madaraka mikoani ni kuona kuwa maendeleoyanawafikia vyema wananchi wa chini hasa kwa kusogezewa huduma za kijamii karibu nao.

Katika kipindi hicho baadhi ya majukumu ya Wizara za sekta za Elimu, Kilimo na Afya, yamehamishiwa katika ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mamlaka hizo zimedhihirisha uwezo wake kwa kufanikisha mambo mbalimbali ikiwemo Huduma za jamii.

Katika kuendeleza azma ya serikali ya awamu ya saba imeonesha dhahiri ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi zikiwemo afya, elimu na maji ambavyo kwa kiasi kikubwa vimeweza kupiga hatua.