GABORONE,BOTSWANA

MAOFISA  wa wanyamapori nchini Botswana wanafanya uchunguzi kuona ni ugonjwa gani uliosababisha karibu tembo 400 kufa katika Delta ya Okavango ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Taarifa hiyo iliripotiwa na vyombo vya habari mbalimbali vya ndani, na vya kimataifa huku maofisa wa wanyamapori wakisema,wizi wa pembe na ndovu na sumu si sababu ya vifo vya mamia ya tembo hao.

Akitangaza habari hiyo kaimu mkurugenzi wa idara ya Wanyamapori na Hifadhi za Taifa wa Botswana Cyril Taolo, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba,walipokea taarifa ya kufa tembo 356 katika eneo la kaskazini mwa nchi (Botswana) la Delta ya Okavango na idara ilithibitisha vifo vya ndovu 275 hadi hivi sasa.

Kwa upande wao, madaktari walisema vifo vya tembo hao havikusababishwa na ugonjwa wa kimeta (anthrax). 

Wataalamu walisema,magonjwa yaliyomo kwenye udongo ambayo mara nyingi yalikuwa yakiua wanyama wengi, huenda ndiyo sababu ya vifo hivyo. 

Mwaka jana 2019 zaidi ya ndovu 100 walikufa katika kipindi cha kiangazi nchini Botswana.

Botswana ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya tembo duniani,Ingawa hata hivyo idadi ya wanyama hao inazidi kupungua katika nchi za chini ya Jangwa la Sahara kutokana na biashara haramu ya meno ya tembo. 

Sasa hivi Botswana inakadiriwa kuwa na tembo laki moja na 30 elfu ambayo ndiyo idadi kubwa zaidi ya wanyama hao kuweko katika nchi moja duniani.

Tatizo kubwa lililojitokeza baada ya kuongezeka sana idadi ya tembo kwenye miaka ya 1990 ni vita baina ya wanyama hao na wakulima kutokana na kukosekana sehemu za kutosha za malisho. 

Hali kwa wakulima ilikuwa mbaya kiasi kwamba mwaka jana,Rais Mokgweetsi Masiri wa Botswana alifuta marufuku ya kuwindwa na kuuliwa tembo.