BERLIN, UJERUMANI

GAZETI  la Ujerumani, Die Welt limeripoti kuwa nchi hiyo imewachukua wahamiaji 10,000 kutoka kwenye kambi za wakimbizi za Uturuki katika miaka minne iliyopita kama sehemu ya mkataba wa wakimbizi kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki.

Gazeti hilo liliripoti kwamba Ujerumani iliwachukua wahamiaji wengi zaidi ikilinganishwa na nchi nyengine.

Takwimu za Halmashauri ya Umoja wa Ulaya zinaonesha kuwa jumla ya wahamiaji 26,835 walipelekwa Ulaya chini ya mkataba baina ya umoja huo na Uturuki kati ya Aprili 4, 2016 na Machi 16, 2020.

Jumla ya wahamiaji 9,967 walikwenda Ujerumani, idadi hiyo ikiwa ni mara mbili ya wahamiaji waliokwenda Ufaransa, inayoshika nafasi ya pili kwa kuwachukua wahamiaji wengi.

Uturuki iliwachukua  wakimbizi milioni 3.6 kutoka Syria. Kwa mujibu wa Die Welt, Uholanzi iliwachukua wakimbizi 4,571, Finland 1,964, Sweden 1,940 na Uhispania 766.