BERLIN,UJERUMANI

SERIKALI kuu ya Ujerumani na serikali za majimbo zimefikia makubaliano ya hatua za pamoja zinazohusu safari za ndani ya nchi. 

Uamuzi huo unakuja baada ya miji miwili katika jimbo la North Rhein Westphalia kurejeshwa chini ya vizuizi kufuatia mripuko mpya wa virusi vya corona. 

Kulingana na makubaliano hayo, watu wanaosafiri kutoka maeneo yaliyo na maambukizo makubwa wataruhusiwa kufikia katika hoteli ikiwa hawana maambukizo. 

Majimbo kadhaa ya Ujerumani tayari yameweka vikwazo kwa wageni wanaotokea katika sehemu zilizoathirika na janga hilo. 

Jumla ya wafanyakazi 1,500 katika machinjio ya wanyama waligundulika kuwa wameambukizwa virusi hivyo na kusababisha miji ya Gütersloh na Warendorf kufungiwa tena. 

Miji hiyo miwili ina takriban wakaazi 628,000. Ujerumani lilikuwa taifa la kwanza barani Ulaya kulegeza masharti yaliyokuwa yamewekwa kuzuia kuenea kwa COVID-19.