BERLIN, UJERUMANI

BARUA zilizoonekana na shirika la habari la Reuters zilisema kuwa mawaziri wakuu wa majimbo manne ya Ujerumani wametoa wito kwa wabunge nchini Marekani kuzuia mpango wa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani.

Mwezi uliopita Rais Donald Trump alisema atapunguza idadi ya vikosi vya majeshi ya Marekani ,Ujerumani kwa 9,500 na wasalie wanajeshi 25,000 tu.

Trump alifikia uamuzi huo baada ya kuikosoa Ujerumani kwa kutofikia lengo la bajeti lililowekwa na jumuiya ya kujihami ya NATO katika masuala ya ulinzi.

Rais huyo wa Marekani pia aliituhumu Ujerumani kwa kuitumia Marekani kwa manufaa yake katika biashara.

Na sasa mawaziri hao wakuu wa majimbo manne yaliyoko kusini mwa Ujerumani ambayo yana kambi za wanajeshi wa Marekani, waliandika barua hizo kwa wabunge 13 akiwemo seneta Mitt Romney.

Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Berlin alikataa kutoa tamko kuhusiana na suala hilo.