NA HAFSA GOLO
TANZANIA sasa imeonesha ukomavu wa kisiasa unaoendana na misingi ya sheria, demokrasia na utawala bora hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa ngazi za urais, wabunge, wawakilishi na madiwani kupitia vyama mbalimbali vya siasa.
Leo hii dunia imeshuhudia hatua kubwa ya kisiasa ambapo karibu vyama vyote tayari vimeshaweka wazi namna ya kuwatafuta wagombea huku baadhi ya nafasi kwa baadhi ya vyama vimeshafunga milango ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za wagombea kupitia vyama husika.
Hatua hiyo bila ya shaka imetimiza malengo ya utawala wenye kufuata demokrasia ya kweli ambapo ni miongoni mwa kichocheo cha maendeleo na kupanua wigo wa fursa sawa kwa wananchi wake.
Ikiwa kuanzia jana hatua ya mchujo wa kuwapata wagombea kwa nafasi mbalimbali kwa chama cha Mapinduzi umeanza takribana nchi nzima bado wagombea wanahaha kujua ni namna gani wanaweza kupenya katika kinyang’anyiro hicho.
Hii inaonesha Dhahiri baada ya kujitokeza kwa wastani wa watangaza nia wapatao 8,000 kwa nafasi za wabunge Tanzania Bara ambapo mahitaji ni wastabi wa watu 394 huku Tanzania visiwani inakisiwa kufikia zaidi ya wagombea 50O hatua ambayo ni ukomavu wa kidemokrasia.
Bila ya shaka dhana ya serikali zote mbili zinazoongozwa chini ya chama tawala cha Mapinduzi (CCM) takribani kwa miaka 43 sasa.
Kama hivyo ndivyo ilivyo, serikali hizo zipo makini katika kusimamia kwa vitendo suala hilo ambalo limeondosha ubaguzi wa dini, rangi, kabila sambamba na kupanua wigo wa kuheshimu maamuzi ya wananchi hasa katika suala zima la kisiasa.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya viongozi wa awamu zote serikalini kufuata kwa vitendo azma ya waasisi wa Muungano na Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliopanua kuzika siasa za chuki na ubaguzi miongoni mwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania Bara kwa ujumla.
Leo nyota njema imeenea na kuangaza kila kona katika pande zote za nchi huku wananchi wakiondokana n hofu wala hila katika kutumia fursa ya kuchagua na kuchaguliwa.
Ili nchi yeyote iweze kupiga hatua ya kimaendeleo ni lazima kuwe na utawala wa kisheria wenye kutoa fursa sawa na kuheshimu maamuzi ya wananchi.