HATA Zanzibar wapo baadhi ya wanyama baada ya kipindi kifupi kijacho watabakia kuwa historia endapo wasipoekewa mikakati ya kuhifadhiwa.
Kwa mfano imekuwa adimu sana hivi sasa kutembea porini kukutana na kenge, mnyama ambaye anawindwa na anapopatikana hulishiwa mbwa ama baadhi ya vijana kujifanyia supu.
Wapo pia wanaoipenda kuisifia kuwa nyama ya panya buku ni tamu, wengine wanakula popo na wengine hata kudiriki kula kima.
Kuliwa kwa wanyama hao sio tu kutawafanya wapotee, lakini pia ni hatari sana kwa maisha ya wanaadamu hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanyama hao kusabambaza maradhi ya virusi.
Hivi sasa duniani kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayotoka kwa wanyama na kuhamia kwa wanadamu na kwa mujibu wa wataalamu magonjwa hayo yataendelea kuwaandama wanadamu.
Ripoti mpya iliyotolewa na wataatamu wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa endapo kasi ya ulaji wa wanyama pori itaendelea kutarajiwe kusambaa kwa maradhi hasa yanayotokana virusi kutoka kwa wanyama na kwenda kwa binadaamu.
Magonjwa yanayotoka kwa wanyama hadi kwa binadamu ambayo yamekuwa yakipuuzwa yanakadiriwa kugharimu uhai wa watu milioni mbili kila mwaka duniani kote.
Maradhi kama ebola, virusi vya magharibi mwa Nile na Sars ni magonjwa ambayo tafiti zimebainisha kuwa yaliotoka kwa wanyama na kuhamia kwa binadamu.
Kwa mujibu wa ripoti ya waatalamu maambukizi hayo kutoka kwa wanyama hadi kwa bindamu sio ya moja kwa moja.
Husababishwa, kulingana na ripoti ya shirika la mazingira katika umoja wa mataifa na taasisi ya kimataifa kuhusu utafiti wa mifugo, kwa kuharibu mazingira asilia – kwa mfano kupitia uharibifu wa ardhi, utumiaji mbaya wa wanyamapori, uchimbaji wa rasilimali na mabadiliko ya hali ya hewa.
Hii inabadilisha jinsi wanyama na binadamu wanaingiliana.”Katika karne iliopita, tumeona milipuko sita ya virusi vya corona”, alisema Inger Andersen, katibu na mkurugenzi mkuu katika shirika la Umoja wa mataifa kuhusu mazingira.
Katika kipindi cha miongo miwili na kabla ya Covid-19, magonjwa yanayotoka kwa wanyama yalisababisha uharibifu wa kiuchumi uliogharimu kiasi cha dola bilioni 100.
“Alisema kwamba watu milioni 2 katika mataifa yenye kipato cha chini na yale ya kipato cha kati hufariki kila mwaka kutokana na kupuuzwa kwa milipuko inayotokana na wanyama kama vile Anthrax, kifua kikuu cha wanyama na kichaa cha mbwa.
Hizi ni jamii zilizo na matatizo ya kimaendeleo na hutegemea sana mifugo na ukaribu wa wanyama pori.
”Utumiaji wa wanyama pori kwa lengo la kupata nyama kwa mfano umeongeza tatizo hilo kwa asilimia 260 katika kipindi cha miaka 50”, alisema Andersen.
”Tumeimarisha kilimo, kupanua miundo msingi na kuchimba mali asili bila ya kuwajali wanyama pori”, alielezea.
Mabwawa, unyunyizaji na viwanda vinahusishwa na asilimia 25 ya magonjwa miongoni mwa binadamu. Usafiri, uchukuzi na usambazaji wa vyakula umefutilia mbali mipaka na umbali.
Mabadiliko ya hali ya anga yamechangia kwa kusambaa kwa viini vinavyosababisha magonjwa.
Ripoti hiyo inatoa mikakati kwa serikali kuhusu jinsi kuzuia milipuko ya siku zijazo, kupitia kuhamasisha usimamizi endelevu wa ardhi, kuboresha maisha miongoni mwa viumbe tofauti na uwekezaji katika utafiti wa kisayansi.
”Sayansi iko wazi kwamba iwapo tutaendelea kutumia wanyamapori na kuharibu mazingira, basi tutarajie milipuko ya magonjwa kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu siku za usoni”, alisema Andersen.
Ili kuzuia milipuko katika siku zijazo, ni muhimu kulinda mazingira.