PRISTINA, Kosovo

UMATI mkubwa uliokuwa ukishangilia ulimkaribisha nyumbani rais wa Kosovo Hashim Thaci baada ya kurejea nyumbani kutoka Uholanzi.

Rais huyo alihojiwa na waendesha mashitaka katika mahakama maalum ya kimataifa kuhusu madai ya uhalifu uliofanywa wakati wa vita ya 1998-1999 ambayo ilipelekea nchi hiyo kupata uhuru wake kutoka kwa Serbia.

Wafuasi wa Thaci waliokusanyika katika kivuko cha mpakani cha Morine kuingia katika nchi jirani ya Albania walijumuisha mamia ya wanachama wa kile kilichofahamika kama Jeshi la Ukombozi wa Kosovo, ambao walimsifia kamanda wao wa zamani wakiwa na bendera na kuimba nyimbo za kizalendo.

Thaci alihojiwa kwa siku nne mjini The Hague katika Ofisi ya Mwendesha mashitaka Maalum kwa ajili ya Kosovo.

Mahakama hiyo, inachunguza madai kuwa jeshi la Ukombozi wa Kosovo lilifanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu.