SANAA,YEMEN

UMOJA  wa Mataifa umethibitisha habari ya kuuawa watoto wadogo saba na wanawake wawili katika mashambulizi ya anga yaliyolenga makaazi ya raia huko kaskazini magharibi mwa Yemen.

Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya UN nchini Yemen Lise Grande, alithibitisha habari za kutokea mashambulizi mawili ya anga yaliyoua watu tisa na kujeruhi watoto wengine wawili na wanawake wawili katika mkoa wa Hajjah, kaskazini magharibi mwa Yemen.

Ofisa huyo wa UN alibainisha kuwa ni jambo la kusikitisha kwa raia kuendelea kuuawa nchini Yemen wakati huu wa janga la corona, katika hali ambayo chaguo la usitishaji vita lipo mezani.

Harakati ya Ansarullah ya Yemen iliukosoa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia, kwa kulenga makaazi ya raia katika hujuma zake za anga nchini Yemen na kusababisha maafa hayo.

Mkurugenzi wa shirika la Save The Children nchini Yemen Naye Xavier Joubert, alieleza kusikitishwa kwake na mashambulizi hayo na picha za kutisha za maiti za watoto wadogo zikiondolewa kwenye vifusi vya majengo yaliyoshambuliwa kwa mabomu.

Wakati huo huo, , msemaji wa muungano wa kijeshi wa Saudia Kanali Turki al-Maliki anadai kuwa watafanya uchunguzi wa mashambulizi hayo,akisisitiza kuwa kuna uwezekano mkubwa yalifanyika kimakosa.

Hii ni katika hali ambayo, mashambulizi ya namna hiyo ya Saudia na washirika wake dhidi ya Wayemen yaliua maelfu ya raia wasio na hatia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa makimbizi, tokea mwaka 2015.