SANAA,YEMEN
MASHIRIKA ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF na FAO yametoa ripoti ya pamoja yakiitahadharisha dunia kuhusu hali mbaya ya upungufu mkubwa wa chakula nchini Yemen.
Ripoti ya mashirika ya Umoja huo ilisema kuwa hali ya Yemen ni maafa makubwa ambapo mamilioni ya raia wa nchi hiyo wanasumbuliwa na njaa.
Ripoti hiyo ilisema kuwa, Yemen inasumbuliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa njaa kuliko eneo lolote jengine duniani.
Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) pia hivi karibuni liliripoti kuwa, hali ya watu nchini Yemen inasikitisha sana na kwamba Wayemeni milioni 18 wanasumbuliwa na uhaba wa chakula.
Nchi ya Yemen ambayo inaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya miaka mitano ya Saudi Arabia, sasa imekumbwa na changamoto nyengine kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.
Virusi hivyo vinasababisha maafa makubwa kwa raia wa nchi hiyo ambayo sehemu kubwa ya miundombinu yake hususan taasisi za afya kama mahospitali, imeharibiwa kwa mashambulizi ya Saudia na washirika wake.
Nchi hiyo ilivamiwa na Saudia na washirika wake mwaka 2015 na inaendelea kuzingirwa kutokea angani, baharini na nchi kavu.