KATIKA kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu wazazi pamoja na serikali wamekuwa wakiweka jitihada kuhakikisha ndoto za watoto hawa haziishii njiani, lakini jitihada zao zimekuwa zikikumbwa na vikwazo mbalimbali.

Vikwazo ambavyo vinasababisha watoto hawa kushindwa kuendelea na masomo pamoja na kuwakatisha tamaa wazazi na serikali kwa ujumla.  Kikwazo kikubwa kati ya vingi ni mimba za utotoni.

Kutokana vikwazo hivi, kumeibuka mijadala baina ya wazazi, jamii, wadau wa maendeleo pamoja na serikali kuhusu watoto hawa kurudi skuli kuendelea na masomo au wakatizwe masomo na kutoruhusiwa kurudi skuli kabisa.

Utafiti wa Sauti za Wananchi (2016) asilimia 71 ya watanzania wanasema wasichana wapewe fursa ya kurudi skuli kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Asilimia 62 wanafikiri ni vyema watoto warudishwe skuli walizokuwa wakisoma awali baada ya kujifungua.

Asilimia saba wanafikiri wasichana wanaweza kuendelea na masomo wakiwa bado wajawazito wakati asilimia mbili wanafikiri wapelekwe skuli tofauti na ile ya awali wakishajifungua. Pamoja na takwimu hizi kuna wengine pia wanasema wasiruhusiwe kabisa kurudi skuli.

Takwimu ni mawazo ya watanzania mbalimbali, je, tumepata kusikia kutoka kwa wahanga wenyewe? Kiukweli watoto wanapitia magumu hasa pale wanapogundua wamepata ujauzito na ndoto zao zinaenda kuyeyuka.

Huwa wanajaribu kila mbinu kuhakikisha kwamba ndoto zao haziishii njiani, lakini mbinu hizi mara nyingi huwa ni hatarishi juu ya maisha yao.

Watoto hawa hujaribu hata kutoa mimba kwa njia zisizo salama ili tu kuendelea kubaki skuli na kuepuka kufukuzwa nyumbani. Unyanyapaa watakao upata nyumbani, kwenye jamii na shuleni huongeza tatizo.

Wahanga wa mimba za utotoni ni zao malezi wanayoyapata nyumbani hasa wale wa vijijini, waishio katika umaskini na ambao wazazi wao hawakupata elimu kabisa. Wengi katika familia hizi hawana malengo bayana juu ya maandalizi ya mtoto kuwa kielimu.

Malezi wanayopewa watoto wa kike sio ya kuwaandaa kuwa wasimamizi wa utu na maslahi yao bali wanalelewa kuwa waoga ambao hawaruhusiwi kujadili jamabo linalohusu maisha yao hasa mbele za wanaume.

Tujiulize, mtoto ambaye hawezi kujieleza mbele ya baba, mjomba au kaka yake anawezaje kuzungumza na mtu baki ambaye anamtaka kingono?

Tafiti zinaonesha, zaidi ya nusu ya wasichana hao walisema wahusika waliotekeleza ubakaji huo ni watu wenye nguvu/ushawishi kuwazidi. Hawa ni majirani muhimu kwa familia, wenye mamlaka na wengine ni ndugu zao (wajomba, kaka zao, baba, nakadhalika.

Ukweli ni kwamba wengi wao hawana elimu sahihi juu ya haki na wajibu wao na ni wahanga wa matukio ya ubakaji. Sheria zetu zimetamka wazi kwamba kushiriki tendo la ngono na mtoto chini ya miaka 18 ni ubakaji.

Hivyo watoto wanahitaji msaada wa kuwawezesha kujitambua kutoka katika ngazi ya familia, jamii na serikali kwa ujumla kabla na baada ya kupata ujauzito.

Mikakati ya kuwasadia kujitambua ilenge pia watoto wa kiume na si wa kike pekee yao ili tupate jamii yenye watu wenye malengo thabiti juu ya maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Utafiti wa Uwezo (2015) unaonesha kuwa watoto ambao mama zao wana elimu wanafanya vizuri kwenye masomo kuliko wale ambao mama zao hawana elimu.

Ikumbukwe kuwa wanawake ndio wanabeba jukumu la kulea watoto wote wa kike na wa kiume, hivyo kama hawana elimu tutapata taifa lenye watu wasio na malengo juu yao na nchi kwa ujumla.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org