MOSCOW,URUSI

MAREKANI Uingereza na Canada zimeituhumu Urusi kwa kujaribu kuiba utafiti wa chanjo ya virusi vya corona wakati janga hilo likiendelea kuongezeka kote duniani.

Brazil ilitangaza kuwa idadi yake iliyothibitishwa ya maambukizi ilipindukia milioni mbili.

Janga hilo limeuwa zaidi ya watu 585,000 na kuwaambukiza zaidi ya milioni 13.6 na kuuathiri uchumi wa dunia tangu liliporipuka mwishoni mwa mwaka jana na matumaini ya ulimwengu yamegeukia chanjo inayoweza kusitisha janga hilo.

Katika ishara nzuri ya karibuni, vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuwa majaribio ya chanjo inayofanyiwa utafiti na Chuo Kikuu cha Oxford yalionyesha kuwa ilitengeneza kinga ya mwili dhidi ya kirusi hicho.

Lakini saa chache baadaye, Kituo cha Kitaifa cha Usalama wa Mitandao kikasema kundi la wadukuzi kwa jina APT29 liliyalenga maabara ya Uingereza yanayofanya utafiti wa chanjo ili kuiba data muhimu za utafiti.

Marekani, Uingereza na Canada ziliituhumu Urusi katika taarifa ya pamoja ya usalama, madai ambayo Urusi iliyakanusha kupitia msemaji wa Ikulu Dmitry Peskov.