MOSCOW,URUSI

URUSI  na China zimetumia kura ya turufu kulipinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lingeongeza muda wa mwaka mmoja zaidi msaada wa kibinaadamu kupelekwa Syria kutoka Uturuki.

Ujerumani na Ubelgiji,ziliwasilisha azimio hilo ambalo lingeruhusu msaada kuendelea kupelekwa Syria kupitia vituo viwili vya kuvukia katika mpaka wa Uturuki bila ya serikali ya Syria kuingilia kati.

Wanadiplomasia walisema mbali na Urusi na China, nchi 13 wanachama wa baraza hilo zilipiga kura kuipitisha rasimu ya azimio hilo.

Wakati wa mazungumzo,Urusi iliomba muda utakaoongezwa usizidi miezi sita na kwamba msaada huo uruhusiwe kupitia kwenye eneo moja tu la mpaka na sio vituo viwili.

Urusi na China zilipiga kura ya turufu, licha ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa maisha ya raia wa Syria yanategemea msaada unaoingia kupitia mipakani.