NA ARAFA MOHAMED
VIJANA wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar, wametakiwa kuachana na masuala ya makundi, ili kujiepusha na vitendo viovu na badala yake kushirikiana kwa pamoja na kuonesha uzalendo wa Chama chao.
Wito huo umetolewa na aliyekuwa Mwakilishi wa Viti Maalum (UWT) Mkoa wa Mjini, Saada Ramadhan Mwendwa, wakati alipokuwa akizungumza na vijana hao huko Baraza la Vijana (UVCCM) katika ukumbi wa CCM Amaan Mkoa.
Alisema, chama cha Mapinduzi kimeanzisha mabaraza ya vijana kwa lengo la kuweza kukutanisha vijana wote na kuweza kukisaidia chama, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na chama hicho .
Alifahamisha kuwa, Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo ni vyema wakawa wazalendo na nchi yao, na kukipenda chama chao ili kuweza kuleta maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Aidha, Saada aliwasihi vijana kujitokeza kwa wingi kukipigia kura chama hicho, katika uchaguzi Mkuu na kuhakikisha chama cha mapinduzi kinapata ushindi wa kishindo kwa mwaka 2020 .