NA MADINA ISSA

VIJANA Nchini wametakiwa kujiepusha na vurugu wakati wa Uchaguzi na baada ya uchaguzi, ili ufanyike kwa amani na kuweza kumchagua kiongozi atakayeweza kuliongoza taifa.

Wito huo umetolewa na Mwezeshaji wa Mafunzo ya kuendeleza amani kwa vijana yenye lengo la kuendeleza kudumisha amani ya Zanzibar, Dk Mohammed Hafidh Khalifan, mafunzo ambayo yalifanyika katika ukumbi wa Wagonjwa wa akili.

Alisema vijana wamekuwa na wajibu wa kuendeleza amani kwa kuhakikisha wakati wote wanatumia fursa za msingi zilizopo kwa kudumisha Amani, ili iendelee kudumu katika Taifa.

Aidha aliwataka vijana hao kutotumia uwepo wa uchaguzi kujiingiza katika vurugu, kwani kumekuwepo na maisha baada ya kumalizika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

“Vijana nakuombeni kila mukikaa muendeleze uwepo huu wa amani kwani ikipotea haiwezi kurudi tena na nyinyi vijana ndio munaotumika sana kipindi hichi hivyo musiwe watumwa kwa sasa” alisema.

Sambamba na hayo, aliwasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa umakini hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuandika ama kutangaza habari zinazoendeleza amani iliyopo.

Nae Mratibu wa Jumuiya ya ZYF, Almas Mohammed Ali, aliwataka vijana watumie ushawishi waliokuwa nao kwa kuhakikisha kuwa amani inaendelea kudumu katika taifa.