NA HABIBA ZARALI
VIJANA katika Wilaya ya Mkoani, wameshauriwa
kutokubali kutumiwa vibaya na wanasiasa katika
kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu, na badala yake waendeleze kujenga
umoja na ushirikiano.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya hiyo,
Issa Juma Ali, wakati
akizungumza na viongozi wa klabu za mpira jimbo
la Mkoani,
katika hafla ya kukabidhi mipira na jezi kwa
klabu za jimbo hilo zilizotolewa na Mwakilishi, Mmanga Mjengo Mjawiri.
Alisema kwa wakati huu vijana wanapaswa
kupambana na kuumwa
na nchi yao kwa kuangalia mazuri wanayofanyiwa
na kuacha kubabaishwa na wanasiasa.
“Katika kipindi hiki wanasiasa watakuwa na
ushawishi mkubwa hasa kwa
vijana kama nyinyi na kutaka kuwalaghai ili
kuhakikisha wanapata
mafanikio yao jambo ambalo huko mbele linaweza
kuwagharimu kwa
maendeleo yenu,” alisema.
Alisema vijana wana ushawishi mkubwa kwa jamii,
hivyo ni
lazima watumie fursa hiyo kuhakikisha wanakuwa
mabalozi wazuri katika
kuendelea na kudumisha amani iliyopo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa shirikisho la
mpira wa miguu ZFF wilaya
ya Mkoani, Nassor Hakim Juma, alimpongeza
mwakilishi wa jimbo la Mkoani kwa kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo.
“Katika wilaya yetu hii na jimbo letu hili la
Mkoani lina madaraja
tofauti ya mpira wa miguu jambo ambalo kwetu ni
faraja kubwa
kwani inawawezesha hasa vijana kupata ajira,”
alisema.
Kwa upande wake, Diwani wadi ya Mkoani, Samir
Juma Abdalla,
aliwahakikishia wanamichezo wa jimbo hilo kuwa
wataendelea kuwapatia
huduma za michezo bila ya ubaguzi.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kina ilani yake
ambayo inaitekeleza sasa
haiwezi kwenda kinyume nayo na kitahakikisha
watu wote wananufaika bila
ya ubaguzi.
Nao vijana hao walimpongeza mwakilishi kwa
kuendeleza
masuala ya michezo katika jimbo hilo.
Hata hivyo, waliahidi kuvitumia vifaa hivyo
kama ilivyokusudiwa na
kuyafanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa wilaya kwa
lengo la kuleta
mshikamano.
Jumla ya seti saba za jezi na mipira 31 yenye
thamani 800,000, vilitolewa kwa klabu za mpira wa miguu jimbo la
Mkoani.