VIJANA ni taifa la leo na sio la kesho kama ilivyozoeleka, kwani tumekuwa tukiona kwa maisha ya sasa huwezi kufanya jambo bila ya kuwashirikisha vijana.

Ni ukweli usiopingika kuwa tunawaona vijana wakishiriki ama kushirikishwa katika nyanja zote muhimu kama vile kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Aidha nchi mbalimbali tumekuwa tukiwaona vijana kuwa chachu ya mabadiliko jambo ambalo linaweza hata kuwasogeza mbele na baadae kuwa viongozi katika taifa lolote lile.

Kwa mfano hapa Tanzania vijana wamejengewa misingi mizuri ambayo imekuwa ikiwaongoza katika kufikia malengo yao ya baadae.

Leo hii tunathubutu kusema kuwa tusingekuwa na viongozi bora, madaktari bora, wahandisi bora, walimu bora, wanasiasa bora na hata viongozi wa dini bora, wafanyabiashara bora ikiwa kama hatukuwajengea misingi imara ya kufikia hapa walipo.

Tumeziona serikali zote mbili kuanzisha programu mbalimbali zinazowahusu vijana kama vile vijana kuwa idara yao, mabaraza yao na jumuiya mbalimbali ziwe za kisiasa, kijamii na hata kiuchumi sambamba na mambo mbalimbali yanayowahusu.

Tunaamini kuwa lengo la kuwa na mambo haya ni kuona kuwa wanafanya mambo yao kwa kujitegemea na kujiamini zaidi.

Inasikitisha sana kuona kuwa hivi sasa vijana wakijiingiza katika mambo yasiyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, mapombe na mambo mengine yanayokwenda kinyume na maadaili.

Hata hivyo, pamoja na kuwa vijana wana fursa ya kujitegemea lakini bado wanahitaji usaidizi, uangalizi na usimamizi kutoka kwa wakubwa kwa mambo yao wanayoyafanya.

Ili kuona kuwa vijana wanakuwa mstari wa mbele katika nyanja zote, na ndio maana vyama mbalimbali vya kisiasa vikaweka nafasi maalumu kwa vijana kuingia katika ngazi za maamuzi kama vile bunge na baraza la wawakilishi.

Katika uchaguzi huu baadae mwaka huu tunawaomba vijana kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vyao kwani wao watawza kuleta ushawishi katika ngazi hizo za maamuzi.