VIJANA ni taifa la leo na sio la kesho kama ilivyozoeleka, kwani tumekuwa tukiona kwa maisha ya sasa huwezi kufanya jambo bila ya kuwashirikisha vijana.
Ni ukweli usiopingika kuwa tunawaona vijana wakishiriki ama kushirikishwa katika nyanja zote muhimu kama vile kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Aidha katika nchi mbalimbali tumekuwa tukiwaona vijana kuwa chachu ya mabadiliko jambo ambalo linaweza hata kuwasogeza mbele na baadae kuwa viongozi wazuri katika nchi zao.
Kwa mfano hapa Tanzania vijana wamejengewa misingi mizuri ambayo imekuwa ikiwaongoza katika kufikia malengo yao ya baadae.
 Tunathubutu kusema kuwa tusingekuwa na viongozi bora, madaktari bora, wahandisi bora, walimu bora, wanasiasa bora na hata viongozi wa dini bora, wafanyabiashara bora ikiwa kama hatukuwajengea misingi imara ya kufikia hapa walipo.
Tumeziona serikali zote mbili kuanzisha programu mbalimbali zinazowahusu vijana kama vile vijana kuwa idara yao, mabaraza yao na jumuiya mbalimbali ziwe za kisiasa, kijamii na hata kiuchumi sambamba na mambo mbalimbali yanayowahusu.
 Tunaamini kuwa lengo la kuwa na mambo haya ni kuona kuwa wanafanya mambo yao kwa kujitegemea na kujiamini zaidi.

Inasikitisha sana kuwaona vijana wakijiingiza katika mambo yasiyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, matumizi ya pombe, bangi na mambo mengine yanayokwenda kinyume na maadaili.

Hata hivyo, pamoja na kuwa vijana wana fursa ya kujitegemea, bado wanahitaji usaidizi, uangalizi na usimamizi kutoka kwa wakubwa kwa mambo yao wanayoyafanya.

Tatizo kubwa tunaloliona ni kwamba vijana wengi wamepinda kiasi cha kushindwa kuziona fursa ambazo serikali imezitoa hali ambayo inawafanya wabakie vibarazani na kuanza kulalamikia umasikini.

Ukweli ni kwamba maisha katika zama hizi yamebadilika sana, kuna kasi kubwa ya ongezeko la watu, kiasi kwamba serikali kutomudu kumpa ajira kila kijana aliyesoma seuze yule aliyekaa kijiweni.