ILE Zanzibar ya kijani iliyovipatia sifa visiwa vyetu, hivi sasa inatoweka kwa kasi kubwa kutokana na mikono ya binaadamu kuendelea kuihujumu rasilimali ya misitu.

Kwa bahati mbaya tena ni jambo la kusikitisha msitu unaotoweka kwa kasi zaidi ni msitu wa asili, ambapo mababu zetu waliitunza na kuihuwisha. Hata hivyo kizazi chetu kinaumaliza msitu huo.

Msitu wa asili uliotunzwa na kupewa hifadhi na babu zetu, uliweza kutoa matunda mazuri na matamu kama chongoma, pilipilidoria, zambarau, fuu na kadhalika.

Ukweli ni kwamba hivi tunavyozungumza matunda hayo yamekuwa adimu kutokana na miti ya asili iliyokuwa ikizalisha imepungua kiasi cha kukaribia kutoweka matunda na miti hiyo.

Chukulia mfano tu pale ambapo miaka 20 au zaidi iliyopita kama ulikuwa unapakumbuka pahala palikuwa na msitu ulionawiri, hivi sasa eneo hilo msitu umetoweka.

Wahujumu wa msitu walipoona mapanga na mashoka wanayoyatumia kuharibu misitu yanachukua muda mrefu waliamua kuingiza nchini misumeno ya moto, ili iharakishe ukataji wa miti.

Tunaelewa mikakati kadhaa inayochukuliwa na serikali katika kukabiliana uhujumu wa misitu ikiwemo kuzuiliwa kwa matumizi ya misumeno ya moto sambamba na kuzishuhudia doria zinazopigwa maeneo mbalimbali.

Hata hivyo, tahariri hii ina masikitiko makubwa sana kuviona vikosi vyetu vya ulinzi, kuwa ndivyo vilivyo mstari wa mbele katika uhujumu wa misitu ambapo wanatumia misitu hiyo kama kuni.

Kwa mastaajabu makubwa utayaona magari makubwa ya vikosi vya ulinzi kubeba shehena za tani za misitu iliyokatwa kwa ajili ya kuni, hasa kutoka katika msitu ya Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hili vikosi vyote vimekuwa vikihusika na uharibifu wa misitu ambapo wakati mwengine magari hayo hubeba hadi kuni mbichi ambazo zinakwenda kuanikwa makambini.

Tulitegemea vikosi vyetu vingekuwa mstari wa mbele katika ulinzi wa misitu kwa ajili ya manufaa ya vizazi vilivyo sasa na vijavyo, lakini kwa bahati mbaya navyo vinahusika katika kuhujumu misitu hiyo.

Huwa tunaona gari za kiraia kusimamishwa katika vituo vya polisi pamoja na maofisa misitu zikisailiwa kuhusu vibali vya kuni zilizopakiwa, lakini gari za vikosi huwa hazisimamishwi wala kuulizwa chochote. 

Tunataka tukumbushe tu, vikosi hivi haviko juu ya sheria kwenye ulinzi wa rasilimali za misitu na hata sheria nyengine za nchi na kwamba wao kwa kazi zao wanatakiwa wawe wasimamizi wa sheria zote ikiwemo ya ulinzi wa misitu na sio kinyume chake.

Kwa jinsi magari ya vikosi hivyo yalivyokuwa na uwezo wa kubeba kuni nyingi, hapana shaka pasipochukuliwa hatua mbadala muda wa miaka michache Zanzibar haitakuwa na msitu na hayo matunda pori yatabakia kuwa historia.

Tunafikiri wakati umefika kwa vikosi vyetu vyote vya ulinzi kuhakikisha vinaingia kwenye matumizi mbadala ya nishati ya kupikia badala ya kutumia kuni kama nishati kwa matayarisho ya chakula.