NA ABOUD MAHMOUD
NYIMBO maarufu inayojulikana kwa jina la ‘dhamana’ iliyoghaniwa na mwanamuziki mkongwe mwenye asili ya Asia Chaganlal Keshavji akiwa kundi la Culture Musical Club, imenipa funzo kubwa sana.
Nyimbo hii ilikua na lengo la kuwahamasisha na kuwaelimisha vijana ambao wanapewa nafasi za uongozi, waweze kuzitumia vizuri katika kuleta maendeleo badala ya kuzitumia vibaya nafasi hizo.
Sina lengo la kuizungumzia nyimbo hiyo au kumzungumzia muimbaji, lengo langu ni kuelezea baadhi ya viongozi ambao wamekua na tabia ya kutumia madaraka yao vibaya hususan viongozi wa michezo.
Lakini nataka kuinasibisha nyimbo hiyo na yale mambo ambayo yanatokea hivi sasa, ambayo ndani ya beti za nyimbo hiyo yamezungumzwa kwa kina kabisa.
Katika kipindi cha hivi karibuni viongozi wa klabu hapa nchini wameonekana kujitia dosari kutokana na maneno mabaya wanayoyatumia wakati wanapokuwa mitaani au kwenye vyombo vya habari.
Maneno hayo wanayoyazungumza viongozi hao yanaonekana kuathiri jamii ikiwemo sekta ya michezo, ambayo imekuwa na mashabiki wengi hususan mchezo wa soka.
Kwa kweli unapokua kiongozi ni vyema kuhakikisha nafasi yako katika jamii iko vipi, na nini utaweza kuzungumza ambacho kitasaidia jamii kukufahamu na kuleta maendeleo ya mchezo wa soka.
Tuseme ukweli viongozi wa klabu za soka wamekuwa hawajielewi na wala hawazijui nafasi zao, katika klabu na kwenye jamii ya ulimwengu wa mchezo kutokana na kuvuka mipaka ya kazi zao.
Tumeshuhudia viongozi hao wakipigishana kelele na viongozi wakuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kwa kuwalaumu kupitia vyombo vya habari na hata mitaani jambo ambalo linawavunja moyo viongozi hao.
Hilo sio jambo zuri tufahamu kwamba kiongozi yoyote akiwa meneja,katibu au rais wa timu, anatakiwa kujifahamu yeye ni nani na majukumu yake ni yepi yanayomlazimu katika timu yake.
Leo hii viongozi hao wameshindwa kutumia vyeo vyao kwa kukaa meza moja na uongozi wa juu wa soka, kwa kuweza kutatua matatizo mbali mbali yanayohusu mchezo huo na badala yake kuanza kutoa maneno machafu ambayo hastahiki kusikika katika jamii.
Mbali na hilo lakini pia viongozi hao wamekuwa wakikaa katika vyombo vya habari na kuelezea matatizo yao, ambayo yanasaidiwa kutokana na biashara haramu ambazo nchi zote duniani zimekua zikipiga vita biashara.
Kwa kweli sio jambo zuri ni vyema tufahamu kwamba viongozi mna dhamana kubwa katika jamii zenu, hasa maswala ya michezo kwani hao waliokuchagueni waliwaamini vyema imani zenu ziwaridhishe hao waliowachagua.
Unapopewa cheo katika timu lazima unatakiwa uheshimu nafasi uliyopewa na ujiheshimu wewe mwenyewe binafsi, kwani hiyo ni nafasi kubwa katika jamii inayokuzunguka na dhamana ambayo unatakiwa uitumie uzuri.
Ni yema viongozi wa klabu kuiga mfano wa viongozi wenzao wa miaka ya nyuma, ambao walikuwa wakiheshimika na wachezaji wao pamoja na mashabiki wa timu, lakini pia walikuwa wakizitumia nafasi zao inavyotakiwa kwa maslahi ya timu.
Hivi ndivyo inavyotakiwa, tuzitumie nafasi zetu za uongozi kwa heshima sio kupita kuzungumza maneno ambayo hayana maana wala umuhimu katika jamii, zaidi ya kubomoa soka la nyumbani na kujitia aibu.
Kama kuna tatizo linalotokea malizaneni wenyewe viongozi wa klabu na shirikisho na kama kuna shida ambayo inahitaji msaada pia nendeni huko ili muweze kusuluhisha hilo.
Kutoka na kwenda kwenye vyombo vya habari kusema mambo yaliokuwa hayana maana ambayo kwa uhakika yataikera jamii,serikali na hata dunia ni jambo la kukemewa sana.
Hakuna sifa ya kubadilika mtu au watu bila kujifunza, kwa sababu kuna watu hawajui kama wanalolifanya ni tatizo na ukiwafunza huwa wanakubali na wanaelewa.
Lakini kuna wengi nao hawajui lakini ukiwaelekeza ama kuwafahamisha wanakuona wewe ndo hujui, hivyo ni vyema kufahamu makosa mnayoyafanya viongozi wa soka kwa maslahi ya soka na taifa.
Wengi tumewaona walianza uongozi kwenye klabu vya michezo na baadae kupata nafasi kubwa serikalini, hii inatokana na utendaji wao mzuri na busara walizokuwa nazo tangu wakiwa kwenye nafasi za chini.
Hivyo kama tunataka kufika mbali katika nafasi za uongozi tuige mifano hiyo ya viongozi waliopita na tuache maneno mengi ambayo baada ya kujenga yanaboa na kuleta athari kubwa kwenye jamii yetu.