NA ARAFA MOHAMED

WAHADHIRI na Wakufunzi wa Vyuo Vikuu nchini wamehimiza kutumia njia za kisasa za ufundishaji, ili kuwawezesha wanafunzi kunufaika na elimu inayotolewa katika Vyuo mbali mbali.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa (Namafoundation) Mfaume  Mtarachapa Juma,  wakati wa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo Wahadhiri na wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar University (Z.U) yaliyofanyika katika tawi la chuo hicho huko Mpendae Mjini Unguja.

Alisema, kupatiwa Mafunzo kwa walimu hao itasaidia kuwafundisha vizuri wanafunzi wa Chuo hicho, ili waweze kunufaika na kupata mambo mbalimbali yanayo husu elimu kwa njia ya vitendo na kinadharia.

Aidha Mwakilishi huyo, alifahamisha kuwa, kupatiwa kwa Mafunzo hayo kutasaidia kumuwezesha mwanafunzi kuwa na ujuzi alioupata kutoka katika Chuo husika.

“Lengo la kupata program hii ni kuleta mabadiliko, ya namna gani profesa anaweza kutumia  ujuzi aliokuwa nao utamfikia mwanafunzi, na uwezo wa kutumia ujuzi anaoupata”alisema.

Rukaiya Wakif Mohamed, Mkufunzi kutoka Chuo hicho alisema, mafunzo hayo watamsaidia na kufanikisha elimu yake kwa kuwafundisha wanafunzi katika mafunzo hayo mapya ya ufundishaji.

“Kiukweli tulikuwa tunafundisha kabla ya ujuzi lakini tulipokuja hapo yumejuwa kuwa taaluma na ujuzi unakuja baada ya mwanafunzi kuwa na nidhamu”alisisitiza.

Akizungumzia kwa upande wa mbinu za kisasa ambazo zitatumika kufundishia chuoni hapo Dokta Khatib Makame Omar, alisema, amefarijika kwa kupewa mafunzo hayo katika chuo chao na kuwafundisha mbinu za kuendelea kusomesha.