NA ABOUD MAHMOUD

WAANDISHI wa habari wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar wametakiwa kujisomea ili kuongeza uwezo wao na kufikia malengo ya shirika hilo.

Akizungumza na waandishi hao jana wakati wa kikao cha asubuhi katika ofisi za shirika hilo ziliopo Kikwajuni mjini hapa, Mwandishi Mkongwe Zanzibar Salim Said Salim alieleza kuwa kufanya hivyo pia kutaongeza ubora wa kazi zao.

Salim ambae pia ni mjumbe wa bodi wa shirika hilo, alisema ili mwandishi awe mzuri katika kazi zake anatakiwa ajitahidi kubadilika badilika katika kazi zake kufikia malengo aliyokusudia.

Aidha aliwataka kukubali kukosolewa na kuelimishwa ili kuondokana na mambo yanayoweza kuzorotesha utendaji lakini pia kupunguza kasi ya kuandika habari nzuri zinazoelimisha jamii.

“Ninawashauri mjitahidi sana katika kazi zenu mpende kujifunza Zaidi, hii itakusaidieni kuwa imara na wabunifu lakini pia kuandika habari nzuri zitakazonufaisha jamii nzima,” alisema maalim Salim.

Aidha Mjumbe huyo aliwataka waandishi hao kujifunza zaidi kwa kufuatilia vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa ili kupata mbinu mbali mbali za kiuandishi.

 “Tuachane na kuangalia filamu, maigizo au nyimbo muda wote. Vitu hivyo havina umuhimu sana katika kufanikisha malengo yetu ya kuwa waandishi bora na wenye uzoefu,” alieleza.

Aliongeza kuwa kama wanataka kubadilika, ni vyema wakaongeza jitahada lakini pia kuangalia waandishi wa vyombo vya habari vyengine ili kuongeza mbinu za uandishi na kufanya mahojiano.