NA HUSNA SHEHA
MWENYEKITI wa chama cha waanika madagaa wa diko la Mangapwani, Mohammed Omar Makame, ameiomba serikali kuwasaidia kuwatatulia changamoto zinazowakabili ikiwemo ya kuwajengea sehemu ya kuhifadhia mizigo yao.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Zanzibar Leo huko Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Alisema kutatuliwa kwa changamoto hizo kutawasaidia kupata sehemu ya uhakika wa kuanika pamoja na kupata sehemu ya uhakika ya kuhifadhi mizigo yao.
Aidha alieleza kuwa katika kambi hiyo pia wanakabiliwa na tatizo la maji safi na salama na uchache wa vyoo vya kudumu katika eneo hilo jambo ambalo linahatarisha usalama wa afya zao.
“Tatizo hili tumeshalipeleka ofisi za halmashauri ya wilaya hadi mkoa lakini bado limekuwa likiendelea, hivyo tunaomba kusaidiwa ili tufanye kazi zetu kwa Amani Zaidi,” alisema.
Mbali ya hayo pia aliomba kuangaliwa upya bei elekezi kama iliyowekwa katika zao la mwani na kuwashauri wapishi wa dagaa kuweka mfumo wa kutumia majiko ya gesi ili kuhifadhi mazingira.
“Miti imekuwa ikihujumiwa sana hivi kutumia nishati ya gezi itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira ya ukataji wa miti ovyo,” alisema.
Naye Subira Faki Kombo alisema kuwepo kwa ghala la kuhifadhia mizigo kutawanufaisha waanika madagaa hao na kuondokana na tatizo la wizi wa vitu vyao wanavyofanyia kazi.
Hivyo aliiomba serikali kuliangalia suala hilo ambapo kazi hiyo inawasaidia kukidhi mahitaji ya familia zao ambapo wengine wamekuwa na hali ngumu na ni wajane.
Pamoja na hayo, waliiomba serikali kuwapatia mikopo isiyokuwa na riba ili kuwasaidia kujinyanyua zaidi kimaisha kwa kufanya biashara itayoweza kuwanyanyua zaidi na kujiendeleza kimaisha bila ya kuhitaji msaada.