NA HUSNA SHEHA
MWENYEKITI wa chama cha waanika madagaa wa diko la Mangapwani, Mohammed Omar Makame, ameiomba Serikali kutatua changamoto zao zinazowakabili wafanya kazi wa chama hicho ikiwemo kuwajengea sehemu ya kuhifadhia mizigo yao (Godauni).
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Zanzibara Leo, huko Mangapwani Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, ambapo alisema kutatuliwa kwa changamoto hiyo kutawasaidia waanika madagaa kupata sehemu ya uhakika wa kuanika pamoja na kupata sehemu ya uhakika ya kuhifadhi mizigo yao.
Aidha alieleza katika kambi hiyo pia wanakabiliwa na tatizo la maji safi na salama pamoja na uchache wa vyoo vya kudumu katika eneo hilo, kwani hivi sasa wameshalipeleka ofisi za Halmashauri ya Wilaya hadi Mkoa, lakini bado limekuwa likiendelea hivyo.
Mbali ya hayo pia aliomba kuangaliwa upya bei elekezi kama ilivyokuwa imewekewa zao la mwani na alishauri wapishi wa dagaa kuweka mfumo wa kutumia majiko ya gesi, ili kuhifadhi ukati wa miti na kuepusha kuwa jangwa na upungufu wa hewa ya Oxygen.