LUSAKA, ZAMBIA
WAZIRI wa Afya wa Zambia, Chitalu Chilufya, amesema baada ya zoezi la lazima la upimaji wa virusi vya corona katika bunge la nchi hiyo, wabunge 15 wamekutwa na maambukizi.
Amri ya upimaji huo ilitolewa baada ya wabunge wawili kufariki dunia juma lililopita.
Mmoja miongoni mwa hao aliugua ugonjwa wa COVID-19, hadi kipindi hicho bunge la Zambia lilikuwa na Wabunge 158.
Katika hatua nyingine Msemaji wa Serikali ya Kenya Cyrus Oguna pia amethibitishwa kuwa na virusi vya corona.
Katika ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa aliona dalili na kwa sasa anapatiwa matibabu katika eneo alilojitenga.
Nchini Afrika Kusini mawaziri wawili walifikishwa hospitali baada ya kupata maambukizi.
Hadi wakati huu Zambia ina visa 3,584 vya maambukizi, wakati Kenya 15,601. Shirika la Afya Dunia WHO hivi karibuni lilionya kutokana na kuchelea kuanza kwa mripuko huo barani Afrika visa vyake katika kipindi hiki vinaongezeka kwa kasi.