NA ZAINAB ATUPAE
WADAU na wapenzi wa soka Zanzibar wamekerwa na hatua ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kuzifutia matokeo timu kwa madai ya kupanga matokeo.
Wakitoa masikitiko yao kwa nyakati tofauti walisema maamuzi hayo wanaweza kuleta migogoro mipya ambayo ilikuwa imesahaulika kwa kipindi kirefu.

Walisema suala la kupanga matokeo ni jambo nyeti ambalo linahitaji ushahidi uliokamilika, kinyume na hapo timu inaweza kukosa imani na kuhisi imeonewa.
“Si dhani kama kuna timu iliyopanga matokeo kwani kila kitu kinaonekana dhahiri, lakini hapa sasa nadhani tujiandae kwa vurugu kubwa ambazo zinaweza kujitokeza katika shirikisho hilo”walisema.

Juma Makame Alawi ,alisema maamuzi yaliyotolewa yanaweza kuchafua soka la Zanzibar, katika hatua za mwisho.
Thuwaiba Abudu’ Chubela’,aliwataka viongozi kuwa makini wakati wanapotoa maamuzi ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.

Aliwataka viongozi hao kutambua timu zilikubali kumaliza ligi katika hali ngumu,hivyo vyema wakaongoza kwa misingi ya kutoa haki kwa kila timu.
Mohamed Salah,alisema anasikitishwa na maamuzi yanayotolewa na viongozi wa soka, ambao wanashindwa kuelewa wanachokifanya.

Abdalla Issa Omar alisema ZFF ya sasa inaonekana kufeli kuongoza soka, pia wanashauriwa kujitathimini ili kuokoa soka .
“Tuseme ukweli kwa haya ambayo yametokea basi hatuna uongozi katika miaka yote, lakini uongozi huu umefeli na unatakiwa kujitathimini au kuondoka kabisa”alisema.
Michezo iliyofutwa matokeo ni Mafunzo na Jang’ombe Boys,KMKM na Jamhuri, Chuoni na Mwenge na Malindi na Jamhuri.