NA HAJI NASSOR

WADAU wa zao la karafuu kisiwani Pemba, wamependekeza kikosi kazi cha kudhibiti magendo ya zao la karafuu, kikaondolewa na huduma zilizokuwa kikipewa na kuhamishiwa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM).

Walisema pia huduma zilizokuwa zikigharamia kikosi hicho sio vibaya kama zitahamishiwa kwa mnunuzi mkuu wa zao la karafuu Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) ili awe na uwezo wa kuwaongezea bei wakulima wa zao hilo.

Wakizungumza kwenye mkutano wa siku moja uliyotayarishwa na Jumuiya ya wazalishaji wa zao la karafuu Zanzibar kwa kushirikiana na mwamvuli wa asasi za kiraia Pemba (PACSO), wenye lengo la kukusanya maoni juu ya kuimarisha zao la karafuu, uliyofanyika Chake-Chake.

Wakitoa maoni yao juu ya sheria namba 2 ya mwaka 2014 ya maendeleo ya karafuu, walisema kikosi kazi ambacho kipo kisheria, hakiwanufaishi wakulima wa zao la karafuu.

Walisema kikosi kazi hicho hutengewa fungu la fedha kwa ajili ya kazi ya kuhakikisha karafuu haisafirishwi magendo lakini kazi kama hiyo inafanywa na KMKM.

Walieleza kuwa kikosi hicho ndicho kinachopaswa kutengewa fungu kubwa zaidi la fedha kutoka serikalini na kupewa vifaa vya kisasa ili kuhakikisha kina uwezo wa kuzifikia bandari zote bubu na kuzia zao hilo lisisafirishwe kimagendo.

Mmoja kati ya wadau hao, Kassim Ali Sagafu wa shehia ya Mtambile, alisema ni vyema kifungu cha sheria kinachotambua kikosi kazi kikafutwa.

“Mimi nahisi katika kuhakikisha fedha za serikali hazipotei ni vyema kwanza kikosi kazi ambacho hutengewa fungu kubwa la fedha, kiondolewe na fedha hizo wapewe KMKM ili kununua boti za kisasa kwa ajili ya kulinda mipaka yetu,”alieleza.