WASHINGTON,MAREKANI

MAELFU  ya wafanyakazi wa Marekani wamegoma kazi na kufanya maandamano wakipinga dhuluma na ukosefu wa usawa.

Waandamanaji katika maandamano hayo yaliyopewa jina la “Mgomo kwa Ajili ya Maisha ya Watu Weusi”, walitaka kuboreshwa hali ya ajira na mazingira ya kazi ya Wamarekani weusi. 

Maandamano hayo yaliyofanyika  katika zaidi ya miji 24 ya Marekani yalitayarishwa na jumuiya za wafanyakazi na taasisi za kutetea haki na uadilifu wa hali zote .

Watayarishaji wa maandamano hayo walitangaza kuwa, wapinzani wa dhuluma na ukosefu wa usawa ambao hawakuweza kushiriki kwenye maandamano walinyamaza kimya kwa dakika kadhaa kuwaenzi na kuwakumbuka Wamarekani weusi waliouawa kikatili na polisi wa Marekani.

Mjini New York, maelfu ya waandamanaji hao walikusanyika mbele ya Hoteli ya Kimataifa ya Trump na kutangaza upinzani wao dhidi ya ubaguzi wa rangi unaofanyika kwa mpangilio maalumu na ukosefu wa usawa wa kiuchumi nchini Marekani.

Wamarekani walikuwa wakifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakipinga ukatili wa polisi na ubaguzi wa rangi.

Maandamano hayo yalianza baada ya polisi mzungu kumuua Mmarekani mweusi, George Floyd  tarehe 25 Mei katika mji wa Mineapolis.