NA ABOUD MAHMOUD

WAFANYAKAZI wa taasisi binafsi wameshauriwa kujiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ili waweze kupata mafanikio wakati watakapostaafu.

Ushauri huo ulitolewa na Mwanasheria wa ZSSF, Ramadhan Juma Suleiman, wakati akitoa mafunzo ya kujiunga na mfuko huo kwa wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya ya kati, Dunga.

Alisema ni vyema wafanyakazi kukubali kujiunga na taasisi hiyo ambayo iko mstari wa mbele katika kuwasaidia wastaafu.

Alifahamisha kwamba mbali na mfuko huo kutoa kiinua mgongo kwa wastaafu pia kuna faida mbali mbali kwa wanachama ikiwemo mkopo wa elimu, mkopo wa kuanza maisha, mafao ya uzeeni na ulemavu.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Salha Mansour Said ambae ni muajiriwa mpya wa taasisi hiyo, alisema mafunzo waliyoyapata yamewapa mwanga wa kufahamu umuhimu wa kujiunga na taasisi hiyo.

Mfanyakazi mwengine Saida Abdulrahman Saleh, alisema kupitia mafunzo hayo amefahamu umuhimu wa mfuko wa ZSSF kwa wanachama.