NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

WAKATI vikao vya kuwachuja watia nia za kugombea nafasi ya ubunge, msakada wawili kati ya 434 wa CCM waliochukua fomu mkoa wa Arusha wameshindwa kurejesha fomu zao na hivyo kupoteza sifa ya kuwa wagombea.

Katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Mussa Matoroka alisema kuwa wanachama wengi wamejitokeza kwenye mchakato wa kuchukua fomu na kurejesha ambao umekamilika leo majira ya saa 10.00 alasiri.

Alisema kuwa katika wilaya ya Arusha wanachama 91 wamejitokeza kugombea nafsi hiyo baada ya mgombea mmoja kushindwa kurudisha fomu wakati wilaya ya Monduli ina wagombea 24 baada ya mgombea mmoja kushindwa kurudisha fomu.

Alisema wilaya ya Longido ina wagombea 12, Wilaya ya Ngorongoro ina wagombea 14 Wilaya ya Karatu ina wagombea 53 Arumeru magharibi ina wagombea 61 na Arumeru mashariki inawagombea 33.

Katibu huyo alisema kundi la Vijana lina wagombea 30, Jumuia ya Wazazi wagombea 9 na kundi maalumu la UWT ambalo linahusisha Watu wenye ulemavu, Wasomi, taasisi zisizo za serikali (NGOs), Wafanyakazi lina wagombea 105 na kufanya kundi maalumu la Jumuiya za chama kuwa na wagombea 114.

“Kwa mujibu wa ratiba kura za maoni ndani ya chama zitafanyika kwa muda wa siku mbili mfululizo yaani Julai 20 na 21 ambapo kila jimbo litakuwa na siku moja tu,” alieleza Katibu huyo.

Alieleza kuwa Julai 23, kutafanyika  mkutano mkuu wa UWT kwa ajili ya kupata wabunge wa Viti maalumu na kufuatiwa na  mkutano mkuu wa UWT wa wilaya utakaofanyika Julai 25 kwa ajili ya kupata madiwani viti maalumu kwa kata zote 158 za mkoa huo.

Amesema Julai 30 kutafanyika mkutano wa baraza kuu la Vijana kwa ajili ya kupata wabunge kupitia kundi hilo na kufuatiwa na mkutano mkuu wa baraza la Jumuia ya wazazi utakaofanyika Julai 31 kwa ajili ya kupata wabunge.

Aidha katibu huyo aliwataka wagombea wote waliorejesha fomu kufanya kampeni za kistaarabu bila ya kuchafuana wala kupakana matope kwa kuwa watia nia wote wana sifa za kuteuliwa kushika nafasi wanazoziomba.