NA HAFSA GOLO

MKUU wa Mapato na Usimamizi wa Madeni Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Asya Abdusalam, amewataka wahitimu wa kidadu cha sita kuwa makini, kujitambua, na kuuthamini utu wao wakati wakisubiri matokeo ya mitihani, ili watimize malengo waliojiwekea. 

Aliyasema hayo kwenye sherehe ya mahafali ya 19 ya kidato cha sita ya skuli ya sekondari Benbella yaliofanyika ukumbi wa skuli hiyo.

Alisema, iwapo wanafunzi hao watakuwa mstari wa mbele kutimiza maadili na heshima pamoja na  kupanua wigo wa kutumia teknolojia zitakazosaidia kuongeza ufanisi wa kujifunza zaidi.

Aidha, alisema, iwapo mwanafunzi wa kike atapiga hatua nzuri ya elimu upo uwezekano wa kuwa balozi mzuri ndani ya jamii pamoja na kuleta maendeleo nchini.

Mkuu huyo, aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha  wanaendelea kuitumia vyema elimu ya ujasiriamali waliopatiwa skulini hapo kwani itakuwa ni sehemu  ya kuwajengea uwezo wa kujiajiri wenyewe.

Aliwataka wahitimu wao wakati watapokuwa vyuoni wahakikishe wanashirikiana karibu sambamba na kubadilishana uzoefu huku wakihimizana umuhimu wa kufuata taratibu na maelekezo wanayopatiwa na viongozi wao.

Alifahamisha kwamba mashirikiano ndio suala muhimu litakalowasaidia kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na ndoto zao.