NA MWANDISHI WETU

WAISLAMU wote duniani wamo katika siku 10 tukufu za mwezi wa Dhul-Hijja, ambapo pamoja na ibada nyengine lakini katika kipindi hiki waislamu wanatekeleza ibada ya funga za sunna ikiwa mahujaji wako Makka nchini Saudi Arabia.

Allah Mtukufu ameziapia siku hizi 10 ndani ya kitabu chake kitukufu cha Qur’an pale aliposema: “Naapa kwa alfajiri. Na kwa siku 10.” [Qur’an, 89:1-2].

Wanazuoni wengi wa tafsiri ya Qur’an wamesema kilichoapiwa katika aya hii ni siku 10 za mwanzo wa Dhul-Hijja, yaani Mfungo tatu, na mtazamo huu pia wameusema Ibn Jariri Twabariy na mwenzake Ibn Kathir (Allah awarehemu Wote).

Siku 10 hizi zinajumuisha ndani yake fadhila na baraka mbalimbali, kutenda amali njema katika siku hizi ni bora kuliko amali njema katika siku nyingine za mwaka, kama alivyotuambia Mtume (S.A.W) “Hakuna siku amali inakuwa bora zaidi kushinda siku hizi 10 za Dhul-Hijja (Mfunguo tatu).”

Maswahaba wakasema: “Hata amali ya Jihad?” Mtume (S.A.W) akasema: “Hata Jihad, ila mtu aliyetoka Jihad akaiweka rehani nafsi yake na mali yake, na kurejea bila ya chochote.” [Bukhari].

Wanazuoni wameitaja hadithi hii kama ushahidi juu ya ubora wa funga ya siku 10 za Dhul- Hijja, isipokuwa haitakikani kufunga siku ya Iddi, kwani kufunga siku hiyo ni haramu.

Sanjari na kufunga, pia ni sharia katika siku 10 hizi kuleta takbira, kwa ushahidi wa hadithi katika Sahihi Bukhari: “Ibn Umar na Abuu Huraira (Allah awaridhie wote wawili) walikuwa wakitoka kuelekea sokoni huku wakileta takbira katika siku 10 za mwanzo wa Dhul- Hijja watu nao huleta takbira kwa kuwafuatishia wawili hao.”