NA WAANDISHI WETU

WAISLAMU nchini wameshauriwa kusheherekea sikukuu ya Eid el Hajj, kwa kula na kuvaa vizuri huku wakimuomba Mwenyezi Mungu kila wakati.

Akitoa salamu za Eid kwa waislamu katika msikiti wa Qadiria Machomanne, Sheikh, Yussuf Ali, alisema waislamu wanapaswa kusheherekea sikukuu hiyo kwa kuvaa vizuri na kula kilicho cha halali.

“Hii leo ni siku tukufu, tunapaswa tusheherekee kwa amani na utulivu pamoja na kula kile kilichokuwa ni cha halali na kuvaa vizuri,”alisema.

Akizungumzia mavazi, aliwasihi wazazi kutowavisha watoto wao nguo zinazoendana kinyume na maadili ya waislamu wakati wanapokwenda kusheherekea sikukuu.

Aidha alisema siku hiyo husheherekewa baada ya kumalizika kwa ibada ya hijja katika mji mtakatifu wa maka, ambapo mwaka huu imefanyika kwa wananchi wanaoishi Saudia tu kutokana na uwepo wa ugonjwa wa corona.

Katika msikiti wa Pembeni Kidutani, Sheikh Ali Hamad Faki, aliwahusia waumini wa dini ya kiislamu kusherehekea sikukuu ya Iddi el  udh–ha, kwa mambo ambayo ameyaridhia Mwenyezi Mungu.

Aliwataka waumini wa dini hiyo kutekeleza sunna ya kuchinja kwa wale wenye uwezo na kuwasaidia wale wasio na uwezo, ili nao waishi kama watu wengine wakiwa na furaha.

“Kuchinja ni sunna kubwa kwa waislamu na hiyo inadhihirisha  nabii Ibrahim, alipooteshwa kumchinja mtoto wake na alipotekeleza agizo hilo Allah akamuokoa kwa kumteremshia kondoo,”alisema. 

Aidha Sheikh Ali Hamad aliwausia waumini hao kuwachunga watoto kwa kuwavisha nguo za heshima jambo ambalo litawaepusha na vishawishi vya udhalilishaji wa kijinsia.

Hata hivyo, alizidi kuwahusia waislamu kutumia mali walizoruzukiwa na mola wao kwa kuzitumia kwa mambo mema ambayo Mwenyezi Mungu ameyaridhia ikiwa ni pamoja na kwenda hijja.

Katika msikiti wa Mtemani Wawi, Sheikh Salum Nasor, katika khutuba ya kwanza alisema waislamu hawajakatazwa kusheherekea kwa kufuata misingi na taratibu ya dini yao.

Aidha aliwataka wazazi kutokuwavisha watoto wao nguo zinazokiuka maadili ambao huwa ni chanzo cha ubakaji kwa watoto hali inayopelekea kurudisha nyuma mustakbali wa maisha yao.

 Hata hivyo, aliwataka waislamu wenye uwezo kwenda makka kuhiji pamoja na kutembeleana na kuwapatia zawadi wagonjwa, mayatima, wajane na wanaishi katika mazingira magumu.