NA KHAMISUU ABDALLAH, DAR ES SALAM

TASISI mbalimbali za serikali ya Mapinduzi Zanzibar, binafsi na wajasiriamali wameshauriwa kushiriki katika maonesho mbali mbali, ili kuweza kujitangaza ndani ya Tanzania na nje ya nchi.

Ushauri huo umetolewa na Ofisa Biashara kutoka Wizara ya Biashara  na Viwanda Zanzibar, Zawadi Zaidu, wakati akizungumza na Zanzibar Leo katika maonesho ya 44 ya Kimataifa jijini Dar es Saalam.

Alisema, ikiwa tasisi hizo zitaweza kushiriki katika maonesho ya aina hiyo wataweza kupata fursa ya kujitangaza na kujulikana huduma zinazotolewa kwa upande wa Zanzibar.

“Watu wengi hawajui tasisi nyingi za Zanzibar zinatoa huduma gani, lakini kuwepo katika maonesho hayo ambayo yana watu wengi basi unaweza kujitangaza kazi tunazozifanya na bidhaa tunazoziuza ikiwemo viungo,” alisema.

Alisema maonesho hayo pia yanaimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, sambamba na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wenzao wa Tanzania bara na kuweza kubadilika.

Alisema kwa upande wa Zanzibar ushiriki  wa tasisi za serikali umeongezeka kutoka sita hadi ikiwemo ZSTC, PBZ, ZURA, ZIPA, ZRB, na wajasiriamali 38 ambao zinazotoa huduma na wafanyabiashara.

Nao washiriki wa maonesho hayo waliipongeza Wizara ya Biashara kutoa fursa kwa taasisi za serikali kushiriki katika maonesho hayo.

Khudhaimat Bakar Kheir ,ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mamlaka ya Udhibiti wa Mamlaka ya Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), alisema maonyesho hayo, kwani ni mara ya kwanza kwa lengo la kuweza kuitangaza tasisi yao na kufahamu majukumu na kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa Zanzibar.