NA MADINA ISSA

KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini Kichama, Abdallah Mwinyi Hassan, amewataka wajumbe wa mkutano wa halmashauri ya majimbo kuwa makini katika kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali katika chama ili ushindi upatikane katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza katika kikao na Makatibu na Wenezi wa majimbo ya Mkoa wa Mjini Kichama huko katika Ukumbi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Jang’ombe.

Alisema, wajumbe hao ndio wenye dhamana ya kuleta kiongozi atakayeweza kuwatumikia wananchi kwa miaka atakayokuwepo madarakani pamoja na kuitekeleza ilani kwa vitendo wakati ukifika.

Aidha alisema ni vyema wajumbe hao kuzingatia alama na kuacha tabia ya kupendelea mtu kwa kumuangalia kwa sura, na badala yake wamuangalie kwa mujibu wa sifa zake ikiwemo kuuzika katika uchaguzi utakapofika.

“Wakati ukifika nakuombeni wajumbe muchague kwa kuwapa alama stahili kwa haki bila ya upendeleo na muache kuangalia udini na ukabila muangalie huyu mtu ataweza kutusaidia kupatikana ushindi katika nafasi anayoiomba” alisema.

Alisema, alama ni vyema kutolewa kwa mujibu wa ibara iliyokuwepo katika katiba ya chama, ili kuendelea kumpa haki yake mgombea wakati ukifika.

Sambamba na hayo, aliwasisitiza wajumbe hao kutunza siri za kikao na kiongozi atakayebainika kutoa siri za vikao hatua ya kinidhamu itachukuliwa kwa mujibu wa kanuni za chama, na kuwasisitiza kila mtu atimize wajibu wake katika majukumu aliyonayo.