ROMA,ITALIA

WALINZI  wa pwani wa Italia wamesema wamewaokoa karibu wahamiaji 100 katika boti la mpira ambalo lilikuwa limejaa upepo nusu nje ya pwani ya Libya baada ya maofisa katika nchi nyengine kushindwa kuingilia kati.

Walinzi hao wa pwani walisema boti hiyo ya mpira inayojazwa upepo ilionekana na ndege mchana katika kanda ya Libya ya utafutaji na uokoaji, SAR, bila ya injini na ikiwa imejazwa upepo nusu.

Mamlaka ya Libya inayohusika na shughuli za utafutaji na uokoaji baharini haikuchukua uratibu wa operesheni za uokoaji kutokana na uhaba wa vifaa vya baharini, kikosi cha ulinzi wa pwani kimesema katika taarifa.

Wahamiaji 84,ambao ni pamoja na wanawake sita na watoto wawili walisafirishwa alfajiri ya jana kutoka katika boti yao ambayo ilikaribia kuzama kwenda katika meli ya Italia, ambayo ilikuwa inaelekea katika kisiwa cha Lampedusa.