KHATIB JUMA, MKOANI

WANANCHI Wilaya ya Mkoani wametakiwa kutokubali kushawishiwa na
wanasiasa kwa  kuvuruga amani iliyopo  nchini,  hasa katika kipindi
hichi cha kuelekea Uchaguzi mkuu wa 2020.

Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mkoani , Issa Juma Ali wakati
alipo tembelea katika Skuli ya Mizingani mkoani Pemba na kuangalia
karatasi zilizo chanwa ambazo zimewekwa na Tume ya uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) kwa ajili ya kuhakiki majina wa waliopoteza sifa ya
kupiga kura.

Alisema kuna baadhi ya watu wasiolipendelea mema Taifa hili wameanza
kufanya uchafuzi wa amani pamoja na kuwashajihisha wengine kwa lengo
la kuleta mifarakano katika jamii.

Alieleza  kitendo cha kuchanwa kwa karatasi zilizobandikwa ni kitendo
cha kihalifu na hakikubaliki kwani kimewakosesha wengine fursa ya
kujiona kama wamepoteza au hawajapoteza sifa, jambo ambalo linaweza
kuleta vurugu hapo baadae.