NA MADINA ISSA

KAMATI ya Maadili na Utendaji ya Chama cha Wananchi CUF, imekaa na kuyapitia majina ya watia nia waliomba ridhaa ya chama chao kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Katibu wa chama hicho, Haroub Mohammed Shaamis, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari, makao makuu ya Chama hicho Darajabovu.

Alisema Ofisi imepokea majina tisa ya waliomba ridhaa ya chama na kuyafanyia uhakiki kuhusu udhamini na malipo na kufikishwa katika kamati kwa hatua nyengine.

Alisema mara baada ya kukaliwa katika kamati, majina yote watayafikisha baraza kuu la Taifa na kupatikana mawili ambayo yatapelekwa katika mkutano mkuu ili kupatikana jina moja ambapo litapeperusha bendera wakati wa uchaguzi kufika.

Hata hivyo, alisema kuwa kwa upande wa mgombea atakayepata nafasi ya kupeperusha bendera kupitia chama hicho, atatakiwa kuendeleza matakwa ya katiba ya chama hicho pamoja na miongozo na kanuni itakayotolewa.

“Imani yetu ni kuona maendeleo yanaendelezwa kupitia chama chetu pamoja na kila mwananchi kumpa haki yake kwa usawa kama chama chetu kinapojielewa ili kila mtu aweze kufaidika na utawala wetu” alisema.